BAGHDAD: Msafara wa magari washambuliwa Iraq
7 Mei 2005
Hadi watu 10 wameuawa katika shambulio jipya lililofanywa kati kati ya mji mkuu wa Iraq Baghdad.Yadhihirika kuwa shambulio hilo lililenga msafara wa magari yaliokuwa na raia wa kigeni.Magari saba yameteketezwa katika shambulio hilo,yakiwemo pia magari matatu ya wageni.Kwa mujibu wa ripoti za wakaazi wa eneo hilo, kulitokea mripuko mkubwa na baadae moshi mweusi ulitapakaa.Machafuko yanayopamba moto yamezusha shaka juu ya uwezo wa serikali mpya kuwashinda waasi.Katika mripuko mwengine mbaya kabisa mshambuliaji aliejitolea kufa kwa kutumia gari lililotegwa bomu,aliuwa si chini ya watu 58 na kujeruhi 44 wengine.Shambulio hilo lilitokea katika mji wa Suwayra,kusini mwa Baghdad ambako Washia wengi huishi.Hapo kabla katika mji wa Tikrit kaskazini mwa nchi,mshambuliaji aliejitolea muhanga maisha,aliripua gari lililotegwa bomu kando ya basi dogo lililokuwa na polisi na kuuwa polisi 9 na kuwajeruhi wengi wengine.Na kaskazini mwa mji mkuu Baghdad,polisi wamekuta maiti 14.Kwa mujibu wa maafisa baadhi ya wale waliouawa walipigwa risasi.Hadi watu 200 wameuawa katika wimbi la mashambulio ya wanamgambo tangu ilipoundwa serikali mpya ya Iraq wiki iliyopita.