BAGHDAD: Mashambulio yaendelea nchini Iraq
7 Mei 2005Mripuko wa bomu lililotegwa kwenye gari,umewaua si chini ya watu 17 katika mji mkuu wa Iraq.Polisi wamesema,bomu hilo liliripuliwa katika njia panda ulipopita msafara wa magari ya shirika la kigeni linalohudumia usalama.Kwa mujibu wa majeshi ya Marekani,miongoni mwa waliouawa ni raia 4 wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi kwenye kampuni ya Kimarekani.Katika siku hizi za nyuma watu mia kadhaa wameuawa katika mfululizo wa mashambulio yaliofanywa sehemu mbali mbali za nchi.Kwa wakati huo huo familia ya Muastralia,Douglas Wood aliezuiliwa mateka nchini Iraq,imewaomba watekanyara wake wamuachilie huru mkandarasi huyo mwenye miaka 63.Hapo awali watekanyara waliipa serikali ya Australia muda wa saa 72 kuanza kuondosha vikosi vyake kutoka Iraq.Waziri wa kigeni wa Australia Alexander Downer amekataa kulitekeleza dai hilo.Australia ina kiasi ya wanajeshi 550 nchini Iraq na hivi karibuni idadi hiyo itaimarishwa kwa askari jeshi wengine wapatao 350.