BAGHDAD. Hali ya usalama Iraq inatisha.
13 Mei 2005Mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga yanazidi nchini Iraq huku habari za hivi punde zinaeleza kutokea shambulizi jingine katika maeneo ya soko mjini Baghdad na ambalo limewauwa yumkini watu 14 na kuwajeruhi wengine 50.
Masaa machache baada ya shambulizi hilo la kwanza bomu jingine lilotegwa ndani ya gari lililipuka upande mwingine katika mji wa Baghdad karibu na msafara wa wanajeshi wa Marekani ambako watu watano wamejeruhiwa.
Mbali na visa vya mashambulizi vinavyotokea kila kukicha waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair amesema ana uhakika kuwa Iraq sasa inapiga hatua kuelekea utulivu na demokrasia.
Wakati huo huo umoja wa mataifa na serikali mpya ya Iraq zimetoa taarifa ya hali ya kimaisha nchini Iraq kufuatia uchunguzi uliofanywa mwaka uliopita na kuzihusisha familia 22,000 kutoka mikoa yote 18 nchini Iraq.
Waziri wa mipango wa Iraq Barham Salih amesema kuwa taarifa hiyo imeonyesha jinsi maisha nchini Iraq si mazuri na moja kwa moja akazielekeza lawama kwa kiongozi aliyeng’olewa mamlakani Saddam Hussein