BAGHDAD: Baraza la mawaziri la Iraq limetimia
9 Mei 2005
Waziri Mkuu wa Iraq,Ibrahim Jaafari ametangaza kuwa baraza lake la mawaziri limekamilika,baada ya bunge la nchi hiyo kuwaidhinisha mawaziri 6 wapya.Lakini Hisham al-Shibli alie Msunni amesema,yeye anaupinga mgawanyo wa madaraka kulingana na madhehebu na atayakataa madaraka yake kama waziri wa haki za binadamu.Wizara muhimu ya ulinzi amepewa Msunni,Saadun al-Dulaimi.Sasa kuna wabunge 17 wa Kisunni katika bunge la wajumbe 275,yakiwepo malalamiko kuwa bunge hilo limedhibitiwa na Washia.Kwa upande mwingine katika mashambulio yaliofanywa sehemu mbali mbali nchini Iraq,wanamgambo wamewauwa wanajeshi 3 wa Kimarekani,2 wa Kiiraqi na afisa 1 wa Kiiraqi.Jeshi la Marekani linasema,wanamgambo 6 wameuawa na wengine 54 wamekamatwa katika msako uliofanywa karibu na mpaka wa Syria.Kwa wakati huo huo Iraq imetangaza kuwa vikosi vyake vya usalama wiki iliyopita,vilimkamata msaidizi mkuu wa mwanamgambo alie mzaliwa wa Jordan,Abu Musab al-Zarqawi.