Bagdad: Mapigano katika mji mkuu wa Iraq.
23 Julai 2006Nchini Iraq hakuonekani mwisho wa matumizi ya nguvu. Huko Kirkuk, kaskazini ya nchi hiyo, si chini ya watu 15 waliuwawa katika mripuko wa bomu lililotegwa ndani ya gari lililoegemezwa katika jengo la mahakama. Karibu watu 50 walijeruhiwa. Na muda mfupi kabla, katika mripuko wa bomu ndani ya gari kwenye mtaa wa watu wa madhehebu ya Shia, zaidi ya raia 30 waliuwawa na wengine 70 walijeruhiwa. Lori lililopakiwa baruti liliripuka karibu na soko. Kwa vile kuna mivutano baina ya Wasunni na Washia, Marekani inafikiria kupeleka wanajeshi zaidi hadi Baghdad. Matumizi ya nguvu baina ya watu wa madhehebu hayo mawili ya dini yamesababisha wasiwasi mkubwa zaidi kuliko mashambulio ya waasi.
Waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, yuko njiani kuelekea Washington kukutana kesho kutwa na Rais Bush, baada ya kusita muda mfupi mjini London ambako atazungumzia juu ya njia za kuboresha usalama mjini Baghdad.