Baerbock aionya Marekani katika ziara yake mjini Kiev
1 Aprili 2025Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amewasili mjini Kiev mapema Jumanne kuonesha mshikamano na Ukraine, katika ziara ambayo haikuwa imetangazwa kwa sababu za kiusalama.
Akianza ziara yake ya kuaga, Baerbock ameionya Marekani isishawishike na mbinu za rais wa Urusi Vladimir Putin katika mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano.
Baerbock ameongeza kusema Ujerumani imeahidi kutoa euro milioni 130 za ziada kama msaada wa kibinadamu na kwa ajili ya kuimarisha Ukraine katika kushughulikia mashambulizi ya Urusi yanayoendelea.
Hii ni ziara ya tisa ya Baerbock nchini Ukraine kama waziri wa mambo ya nje tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi mnamo Februari 2022.
Huenda ikawa ziara yake ya mwisho kama waziri wa mambo ya nje huku Ujerumani ikijiandaaa kuwa na serikali mpya ya mseti kufuatia uchaguzi wa Februari.