Wamarekani kufukuzwa kwa kuyasaidia magenge ya Haiti
23 Julai 2025Marekani inajiandaa kuwarejesha makwao baadhi ya raia wa kigeni wenye vibali halali vya ukaazi wa kudumu kwa tuhuma za kuwasaidia viongozi wa genge la Haiti.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amesema Marekani imebaini baadhi yao waliwasaidia viongozi wa genge lenye mafungamano na kundi lililoorodheshwa na Marekani kuwa la kigaidi.
Katika taarifa yake, Rubio amesema baadhi ya wakazi hao wa Marekani waliwasaidia viongozi wa kundi la Viv Ansanm, muungano uliojihami na silaha unaodhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, ambalo utawala wa rais Donald Trump uliliorodhesha kuwa la kigaidi mnamo mwezi Mei.
Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani ameongeza kuwa wizara ya usalama wa ndani sasa inaweza kuwafuatilia na kuwarejesha makwao, ingawa haijabainikiwa ni wangapi ambao huenda wakalengwa na hakuna majina yoyote yaliyotajwa.
Wizara hiyo ya usalama wa ndani imesema jana Jumatatu (21.07.2025), kwamba maafisa wake wa uhamiaji wamemkamata Pierre Reginald Boulos, aliye na kibali halali cha kudumu cha kubakia Marekani ambae pia ni raia wa Haiti kwa madai ya kujihusisha na vurugu na kuchangia kuiyumbisha Haiti.
UN: Magenge ya Haiti yenye silaha bora yanaendelea kuidhibiti Haiti
Boulos, aliye na miaka 69, anasemekana kuwa mfanyabiashara mashuhuri na mshirika tata wa kisiasa. Hatua ya Rubio inakuja wakati utawala wa Trump kuanzisha wimbi la kuwaondoa wahamiaji haramu nchini humo ili kutekeleza moja ya ahadi za Trump katika kampeni yake ya kuwania urais. Rubio amekuwa akitumia nafasi hiyo kubatilisha visa na hati halali za wanafunzi wanaoandamana kupinga vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Serikali ya mpito ya Haiti hadi sasa haijasema lolote kuhusiana na hatua hii. Takriban watu 500 wameuwawa Haiti kati ya Oktoba mwaka 2014 na Juni 2025 kufuatia vurugu kali zinazosababishwa na magenge ya wahalifu, hii ikiwa ni kulingana na ripoti ya Kamishna Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa.