Baadhi ya familia za mateka zapoteza imani na Netanyahu
21 Julai 2025Hivi karibuni makumi ya waandamanaji walikusanyika mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Duru za habari zinasema taarifa za maandamano hayo zilitolewa ndani ya muda mfupi kabla ya kufanyika kwa sababu yaliingiliana na mikutano ya wanasiasa wa ngazi ya juu wa Israel iliyofanyika kwenye jengo hilo hilo la ofisi ya Waziri Mkuu.
Mikutano hiyo ilijadili yanayojiri katika majadiliano yasiyo ya moja kwa moja na wanamgambo wa kundi la Hamas kuhusu makubaliano ya kusitisha vita ambayo yangewezesha kurejeshwa nyumbani kwa baadhi ya mateka.
Mmoja wa wanaoendelea kushikiliwa na Hamas ni Carmel Gat na mkasa wake unaonesha namna maisha ya mateka yalivyo hatarini Gaza.
Alipaswa kuwa miongoni mwa mateka zaidi ya 100 na wafungwa 240 wa Kipalestina walioachiliwa huru katika makubaliano ya awali ya Novema mwaka 2023. Makubaliano ya kusitisha vita yalipovunjika alisalia mateka Gaza.
Baada ya siku 328 wanajeshi wa Israel walimkuta yeye na mateka wengine watano wa Israel wakiwa wamekufa kwenye handaki kusini mwa ukanda huo.
Ripoti za uchunguzi wa madaktari zilibainisha kuwa Gat aliyekuwa na miaka 40 na wenzake walikufa kwa kupigwa risasi kutoka umbali mfupi.
Binamu wa Gat Gil Dickman, amekuwa mmoja wa wanaopaza sana sauti wakiunga mkono makubaliano ya kuachiliwa kwa Gat na mateka wengine waliosalia.
Ameiambia DW kuwa hata hivyo majadiliano ya kupata makubaliano kama ndoto ya mchana. Anasema kama Netanyahu angelifanya maamuzi sahihi huenda ndugu yake bado angekuwa nyumbani.
Dickman pia anaishutumu serikali ya Israel kuwa inadhibitiwa kisiasa na watu wenye itikadi kali, akimaanisha washirika wa Netanyahu wanaofuata siasa kali za mrengo wa kulia kama vile Waziri wa usalama wa taifa Ben-Gvir na Waziri wa fedha Bezalel Smotrich, ambao wote wanataka Wapalestina waondoke Gaza na walowezi waishi humo. Anasema madhumuni ya viongozi hawa ni pamoja na ardhi na si maisha ya watu na wanayachukulia madhumuni haya kuwa matakatifu.
Familia: Muhimu tupaze sauti zaidi
Kisa kingine ni cha Nimrod, mtoto wa muandamanaji mwingine aitwaye Yehuda Cohen.
Kijana huyo ni kati ya mateka 20 wanaodhaniwa kuwa bado wako hai wakati inaaminika kuwa mateka 30 wamekufa.
Katika mazungumzo na DW, Cohen ameeleza namna alivyokosa imani na serikali ya Netanyahu kuhusu kuwarejesha nyumbani mateka.
Anasema hamuamini Netanyahu, ila anaamini kwamba serikali ya Marekani pekee ndiyo inaweza kumlazimisha Netanyahu kutia saini makubaliano
Anaorodhesha sababu za kutoiamini serikali ya Israel kuwa ni pamoja na kusisitiza kwake kusalia katika njia ya Philadelphi, na wasaidizi wa Netanyahu wanaodaiwa kuvujisha nyaraka za siri gazeti la Ujerumani la Bild, ili kuwa na ushawishi wa maoni umma unayoinufaisha serikali.
Yehuda Cohen, anasema njia pekee ya kumrejesha mwanaye nyumbani ni kuendelea kuwapambania mateka ili waachiliwe na kuvimaliza vita kwa kuzungumza na vyombo vya habari au kuandamana nje ya ofisi ya Netanyahu.