Trump apingwa baada ya kudai kuvimaliza vita vya Kongo
27 Agosti 2025Mnamo Jumatatu ya wiki hii, Donald Trump alirudia madai kwamba ameumaliza mzozo huo uliodumu kwa miongo kadhaa huku akiielezea Kongo kama taifa la Afrika lililoko gizani.
"Nimevimaliza vita saba, vita vilivyokuwa vikiendelea. Vimojawapo vilipiganwa kwa miaka 31 nchini Kongo. Kama mnavyojua, kwa Rwanda, vilikuwa vita vilivyopiganwa kwa miaka 35. Silazimiki kuvizungumzia kwa undani zaidi. Mnafahamu vizuri kuliko mimi."
Amesema kwa miaka 35, watu milioni 9 wameuliwa kwa mapanga na kuongeza kuwa alivimaliza na kuwanusuru watu wengi sana.
Shirika la Associated Press hapo kabla lilifanya uchunguzi ili kuthibitisha madai hayo ya Trump na kugundua kwamba vita hivyo si vya kuisha leo wala kesho.
Hivi sasa wakaazi wa mashariki mwa Kongo wanaripoti mapigano makali katika baadhi ya maeneo, na hasa yakiwahusisha wanamgambo wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda na waliodhibiti miji mikubwa mapema mwaka huu dhidi ya wapiganaji wwanaopambana sambamba na Jeshi la Kongo.
Makubaliano ya mwisho kati ya Kongo na waasi hao yaliyosimamiwa na Qatar yanaonakena ni kama yamekwama, huku kila upande ukimshutumu mwenzake kwa kukiuka masharti ya makubaliano hayo.
Kipi kinachosemwa kuhusiana na madai haya Trump?
Mkaguzi mmoja kwenye shirika la nchini humo linalojihusisha na haki za binaadamu kwenye eneo la Kabare, Jimbo la Kivu Kusini Ciruza Mushenzi Dieudonné, anasema bado wakazi wa jamii za Bugobe, Cirunga, Kagami na Bushwira wanayakimbia makazi yao kutokana na mapigano kati ya waasi wa M23 na wanamgambo wa kundi la Wazalendo.
Amesema, na tatizo kubwa ni kwamba hakuna msaada wa kiutu na watumishi wa afya hufanya kazi mchana na usiku hukimbilia mahali pengine ili kujificha wakihofia usalama wao.
Amnesty International yaripoti mapigano wiki hii
Christian Rumu anayefanya na shirika la haki za binaadamu la Amnesty International ameripoti kwamba makundi ya haki za binaadamu yameshuhudia mapigano katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita kwenye maeneo kadhaa. Akasema, madai ya Trump ya kuvimaliza vita nchini humo hayana ukweli hata kidogo.
Mwanaharakati huyo amesema Rais huyo wa Marekani amepotoshwa katika tathmini yake kwa sababu haki za binaadamu zinaendelea kukiukwa kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu, huku akimsisitiza Trump kufanikisha mazungumzo ya amani.
Trump, "Harakisha mchakato wa amani"
Amani Safari, mwanafunzi wa mjini Goma, ambako waasi wa M23 walichukua udhibiti na ambao umeathirika vibaya kwa vita amesema hakuna kilichobadilika tangu kulipofikiwa makubaliano mwezi Juni. Akasema, Marekani inaangazia zaidi maslahi yake kuliko kuvimaliza vita.
Mwanaharakati wa mji huo wa Goma Espoir Muhinuka, amesema hakuna dalili ya vita hivyo kumalizika hivi karibuni na kumtolea wito Trump kuchukua hatua za kufikiwa makubaliano ya kudumu ya amani na kusitisha mapigano. Amesema kama hilo halitawezekana, ni dhahiri hali ya kiutu itazidi kudhoofika.
Wakaazi wazidi kupoteza matumaini ya amani
Rais wa shirika la kiraia la Kivu Kaskazini John Banyene amesema yeye na wakazi wengine wanapoteza matumaini ya amani ya kudumu. Amesema mauaji, watu kukimbia makazi yao na mapigano vinaendelea, na ni kwa maana hiyo, bado watu wako katika hali ya sintofahamu. Akasisitiza kama vyama vya kiraia, wanahimiza mazungumzo kuendelea, licha ya kwamba yanajikongoja.