Baada ya miaka miwili ya vita Sudan, matumaini ya amani bado
15 Aprili 2025Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Sudan imeingia kwenye hali mbaya sana baada ya vita kuzuka kati ya Jeshi la Kitaifa (SAF) na kundi la wanamgambo wa RSF. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nchi hiyo yenye utajiri wa dhahabu, mafuta na ardhi nzuri, sasa inakabiliwa na moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu na ya wakimbizi duniani. Kati ya watu milioni 51, zaidi ya asilimia 60 wanategemea misaada ya kibinadamu na zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kukimbia makazi yao.
Wanawake na wasichana wa Sudan ndio waathirika wakuu, kwani wengi wao wamepoteza makazi na pia wanakumbana na ubakaji wa halaiki na ukatili wa kingono. Idadi ya vifo bado haijulikani kwa uhakika kutokana na mapigano yanayoendelea, lakini mashirika ya misaada yanasema watu waliouawa wameongezeka kutoka 40,000 hadi 150,000.
Soma pia: RSF yazidisha mashambulizi, vita vya Sudan vikifikisha miaka miwili
Vita hivi vinavyoingia mwaka wa tatu tarehe 14 Aprili vinaongeza uwezekano wa Sudan kugawanyika katika maeneo mawili yenye tawala tofauti. Hager Ali, mtafiti kutoka Ujerumani, anasema hali hii inapunguza matumaini ya kumaliza ghasia hizo. Anasema, "Tunaweza kuhitaji hadi miaka 20 au zaidi kurejesha hali ya kawaida Sudan."
Kwa nini vita vilianza na kwa nini havijaisha?
Mwaka 2021, majenerali wawili —Abdel-Fattah Burhan, mkuu wa majeshi ya Sudan, SAF na Mohamed Hamdan Dagalo, kiongozi wa kundi la RSF — walipindua serikali ya mpito iliyokuwa inajaribu kuleta demokrasia. Mwaka 2023, waligombana kuhusu nani awe na mamlaka zaidi, na hasa kuhusu kuunganisha RSF ndani ya SAF. Mapigano yalianzia Khartoum na baadaye kusambaa nchi nzima.
Hivi sasa, SAF wanadhibiti kaskazini na mashariki mwa Sudan pamoja na mji wa Wad Madani. RSF wamejikita zaidi katika eneo la Darfur. Katika mji wa El Fasher, pande zote mbili zimezingira kambi za wakimbizi, huku raia wakifa kwa njaa na mabomu.
Shirika la International Rescue Committee linasema kuwa hali imekuwa ngumu zaidi kwa sababu makundi mengi yamejiingiza vitani. Hii inafanya iwe vigumu kufikia makubaliano ya amani. Vilevile, baadhi ya nchi jirani na za kimataifa zinapeleka silaha Sudan, jambo linalochochea mapigano zaidi.
SAF wanasaidiwa na Misri na Qatar, huku RSF wakidaiwa kupata silaha kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia Chad. Ingawa UAE inakana, kuna ushahidi wa silaha kutoka huko.
Jamii ya kiraia ya Sudan yazidi kuwa nguzo ya matumaini
Takribani Wasudan milioni 9 wamekimbilia maeneo mengine ya nchi yao, na zaidi ya milioni 3.3 wamekimbilia mataifa jirani kama Misri, Libya, Chad na Sudan Kusini. Huko wanakumbana na matatizo mengi kama ukosefu wa msaada, ukatili na changamoto za viza.
Soma pia: Sudan yaiambia korti ya ICJ kwamba UAE ndio "nguvu inayoendesha" mauaji ya halaiki
Waliobaki nchini wanakumbwa na njaa, ukosefu wa huduma za afya na uchumi ulioporomoka. Bei ya bidhaa imepanda kwa zaidi ya asilimia 140 mwaka huu. Katika hali hii, jamii ya kiraia imekuwa msaada mkubwa. Kuna mitandao ya "emergency rooms" inayosaidia watu kupata huduma za dharura, tiba, na taarifa muhimu. Mitandao hii ilianzia kwenye harakati za kupinga utawala wa Omar al-Bashir mwaka 2019.
Michelle D'Arcy wa shirika la Norwegian People's Aid anasema kuwa vijana na wanawake wamekuwa mstari wa mbele kudai amani huku wakitoa huduma muhimu kwa jamii zao. Hata hivyo, juhudi hizi zimeathiriwa na upungufu wa fedha na uhaba wa nafasi za kiraia.
Alexandra Janecek kutoka IRC anasema kuwa mipango mingi ya kusaidia mamilioni ya Wasudan imefungwa — ikiwa ni pamoja na asilimia 60 yamajiko ya kijamii yaliokuwa yakihudumia watu milioni 2.
Sudan katika janga kubwa la kibinadamu
Umoja wa Mataifa unasema kuwa kati ya dola bilioni 4.2 zinazohitajika kusaidia Sudan mwaka 2025, ni asilimia 6 tu iliyopatikana hadi sasa. Hali imezidi kuwa mbaya baada ya Marekani kupunguza ufadhili wake wa nje, ambao hapo awali ulitoa karibu nusu ya misaada yote nchini Sudan.
Edem Wosornu kutoka ofisi ya misaada ya OCHA anasema Sudan iko "katika janga la kibinadamu lililotengenezwa na binadamu" na bado hakuna dalili ya mwisho.