ASEAN yajadili ushirikiano wa kibiashara na usalama
27 Mei 2025Lengo kuu la mkutano huo ni kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kulinda mataifa wanachama dhidi ya changamoto za kijiografia, pamoja na vikwazo vya ushuru kutoka Marekani.
Akizungumza katika mkutano huo wa 46 wa jumuiya ya ASEAN, Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, ameeleza kuwa uhusiano mzuri kati ya ASEAN na GCC utasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili, kuongeza uthabiti wa kiuchumi, na kufanikisha ustawi wa kudumu.
Waziri Mkuu wa China, Li Qiang, amejiunga na mkutano huu ambao ni mara yake ya kwanza kufanyika kati ya jumuiya ya ASEAN na GCC pamoja na China, hatua inayoonyesha nia ya China kuwa mshirika wa kuaminika katika eneo hilo.
Mwelekeo wa Biashara
Katika hali ya ushindani wa kibiashara, jumuiya ya ASEAN imekuwa na sera ya kuwa huru na kushirikiana na mataifa makubwa kama Marekani na China, lakini ushuru wa Marekani ulioanzishwa na Rais Donald Trump ulisababisha changamoto kubwa kwa baadhi ya wanachama wa ASEAN, ambapo ushuru ulifikia hadi asilimia 49.
China, ambayo imeathirika zaidi na ushuru wa Marekani, inataka kuimarisha ushirikiano wake na ASEAN na GCC ili kuendeleza masoko yake.
Ripoti zinaonyesha kuwa biashara kati ya China na ASEAN imeongezeka kwa kasi, huku mauzo ya China kwenda Thailand, Indonesia na Vietnam yakipanda kwa kiwango kikubwa mwezi Aprili, hali inayotokana na kusafirisha tena bidhaa zilizolengwa na soko la Marekani.
Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim anatarajia kufanikisha mkutano kati ya viongozi wa ASEAN na Rais Trump ili kujadili masuala ya ushuru.
"Hivyo, uhusiano kati ya ASEAN na GCC bila shaka utakuwa muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimaeneo, kujenga uthabiti na kuhakikisha ustawi endelevu kwa wote."
"Majadiliano ya leo yatakuwa ya msingi katika kuhakikisha kwamba ushirikiano wetu unabaki kuwa wa nguvu, wenye mwitiko wa haraka na wenye matokeo mazuri. Tuna uwezo na wajibu wa kuinuka kama nguzo za uthabiti na muelekeo wa ukuaji kwa siku za usoni." Alisema Anwar.
Mzozo wa Bahari ya China Kusini
Licha ya msisitizo wa mshikamano wa kiuchumi, mgogoro wa Bahari ya China Kusini bado unaendelea kuwa suala nyeti. Rais wa Ufilipino, Ferdinand Marcos Jr., amesisitiza hitaji la kutunga kanuni madhubuti za kimataifa kuhusu utawala wa Bahari ya China Kusini, suala ambalo linaendelea kuzua mvutano kati ya China na baadhi ya wanachama wa ASEAN.
Chong Yew Keat, mtaalamu wa masuala ya usalama na siasa katika Chuo Kikuu cha Malaysia, anasema kuwa kuongezeka kwa ushawishi wa China katika eneo hili kunaweza kuifanya Marekani kupunguza usaidizi wake wa kijeshi na kiuchumi katika eneo la Asia-Pasifiki.
Mgogoro wa Myanmar
Katika suala la mgogoro wa Myarmar, viongozi hao walielezea kutoridhishwa na hali ya kisiasa inayoendelea tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021. Waziri Mkuu Anwar alibainisha kuwa jumuiya ya ASEAN inaendelea na mazungumzo ya faragha na pande husika akitaja diplomasia kama njia ya kuleta suluhu ya kudumu katika mgogoro huo.
/AFP, AP