Ardhi ya ekari 100 yatengwa kwa makaburi mapya Nairobi
28 Agosti 2025Wakaazi wa jiji la Nairobi sasa wanashusha pumzi baada ya kupata nafasi zaidi mahsusi kuwapumzisha wapendwa wao wanapomaliza safari ya maisha hapa duniani.
Serikali ya kaunti ya Nairobi imetenga ekari 100 za ziada kutumika kama sehemu ya makaburi ya jiji. Makaburi ya umma ya Lang'ata yalitangazwa kujaa zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Kila wiki familia zisizopungua 30 huwasindikiza wapendwa wao waliohitimisha safari ya maisha yao hapa duniani kwenye makaburi ya Lang'ata.
Makaburi hayo yalitangazwa kuwa yamejaa miaka 25 iliyopita. Ili kuwapa wafu heshima ya kudumu, serikali ya kaunti ya Nairobi imetenga ekari 150 za ziada kwenye eneo la ardhi ya jela la ulinzi mkali la Kamiti na kambi ya jeshi ya Embakasi kutumika kama sehemu ya makaburi mapya.
Makaburi ya umma ya Lang’ata yamejaa
Akizungumza mbele ya bunge la kaunti ya Nairobi, Tom Nyakaba, afisa mkuu wa afya ya umma katika kaunti ya Nairobi alibainisha kuwa maandalizi yanaendelea.
''Sehemu hizi zinaandaliwa na zitaanza kutumiwa kwa maziko katika muda usio mrefu. Sehemu ya Mavoko ya ekari 48 ilinunuliwa kabla ya mfumo wa ugatuzi kuanza. Kwa sasa kila kaunti ina wajibu wa kusimamia operesheni zake za maziko. Madhali ardhi hiyo iko kaunti ya Machakos, hati yake ya umiliki haina jina letu basi tutasubiri magavana husika wafikie mwafaka.''
Afisa huyo wa afya ya umma alipuuzilia mbali madai kwamba kuna ubaguzi wa aina fulani katika mchakato wa kupangia wakaazi sehemu za maziko.
Kaunti ya Nairobi inasimamia operesheni za maeneo tisa ya makaburi yakiwemo ya Wayahudi ya Forest Road, Pangani, Mutuini, Uthiru, Southlands, Kariokor Christian, Ruai na sehemu iliyo karibu na Idara ya Polisi wa Taifa.
Makaburi mengi yanasimamiwa na jamii ila kaunti ya Nairobi, na pia iko mbioni kuimarisha uratibu ili kuondoa utegemezi kwa yale ya Lang'ata. Kwa upande mwengine, kuna mapungufu ya kisheria kuhusu kina cha makaburi, jambo linalozua vurugu na kuathiri mipango.
Kimsingi, hakuna sheria inayolazimu makaburi kuchimbwa kina cha futi sita. Hilo limeisukuma kaunti ya Nairobi kuandaa sheria na sera mujarab. Kuhusu suala la kuzika maiti zaidi ya moja kwenye kaburi moja katika nyakati tofauti, afisa mkuu wa afya ya umma Tom Nyakaba alisisitiza kuwa hilo linakubalika kisheria ila kwa kufuata kanuni za afya.
Suala hilo limezua hisia mseto kwenye bunge la taifa na baadhi wanashinikiza makaburi ya Lang'ata yafungwe. Katibu katika wizara ya afya nchini Kenya, Mary Muthoni anaafiki kuwa upo umuhimu wa kuchukua tahadhari za kiafya.
''Tunataka kulinda na kudumisha afya ya umma hivyo basi kuhusu suala hilo la makaburi tunaunga mkono mapendekezo ya kamati maalum ya kuwa na sehemu nyengine mujarab za maziko.''
Juhudi za kuyahamisha makaburi zimekumbana na vizingiti vya kisheria kama zilivyo harakati za kuipanua sehemu ya maziko ya Lang'ata kwa sababu ya ujenzi wa makaazi binafsi kwenye maeneo ya karibu.
Kwa sasa ada ya maziko Lang'ata ni shilingi alfu thelathini za Kenya, kwa makaburi ya kudumu, na kwa raia wa Kenya. Lakini kwa watoto na yale ya muda, inashuka. Raia wa kigeni wanatozwa ada ya juu zaidi.