APR Mabingwa wa Kombe la Amani Rwanda
5 Mei 2025Fainali hii ya dabi ya Milima elfu moja ilikuwa ikisubiriwa na wengi mno kujua nani bingwa wa mwaka huu.
Mshindi wa kombe la Amani nchini Rwanda hupewa tikiti ya kushiriki kinyang'anyiro cha Shirikisho la soka barani Afrika( CAF Conferations Cup).
Moja kwa moja APR imepata tikiti tayari ya kushiriki mashindano hayo makubwa barani Afrika. APR ina miaka 8 ilikuwa haijatwaa kombe hilo la amani.
Soma pia: APR FC ya Rwanda yanyeshewa mvua ya magoli
Mfungaji wa bao la pili Mugisha Gilbert amesema kwamba walkuwa na hamu sana na hili kombe.
"Tumecheza dabi 3 hapa tukigawana alama baada ya kujadiliana kwa pamoja tumeamua kutumia nguvu zetu zote ili tutwae kombe hili hatimaye imewezekana tunashukuru Mungu."
Romario Abdul Djabari ni mchambuzi wa michezo anaeleza kilichosababisha kushindwa kutamba kwa Rayon.
"Kupata ushindi wa mabao 2 kwa sifuri dhidi ya Rayon niseme kwamba APR walikuwa wazuri hasa kwenye kiungo ambapo walikaba sawa sawa kwa sababu Rayon nguvu zao ziko kwenye kiungo.Ukimpa nafasi Kevin pamoja na wachezaji wa pembeni, inakuwa shida kubwa sana."
Huku zikisalia mechi tano kabla ya ligi kutamatika, timu ya Rayon inaongoza ligi kuu ya soka ikiwa mbele ya APR kwa alama 1.
Mshindi wa ligi kuu ya soka huwakilisha Rwanda katika michuano ya mabingwa barani Afrika (Champions League).
Rayon ilitwaa kombe hili mwaka 2023 ambapo iliipokonya mpinzani wake APR kwa bao 1-0. APR ikiwa na hamu ya kombe hili ililolitwaa mwaka 2018.
Aigle Noir FC mabingwa wa Burundi
Kwengineko, mkoani Makamba nchini Burundi timu ya soka ya Aigle Noir FC imetawazwa mabingwa msimu huu wa 2024-2025, imeipokonya jeshi la Polisi Rukinzo kwa magoli 2-0 kwenye uwanja wa Nkurunziza Peace Park complexe jumamosi.
Fleuri ni mchabuzi kutoka jijini Bujumbura, amesema "Hadi sasa imebaki mechi moja kabla ya ligi kufikia ukingoni timu ya Aigle Noir ndio mabingwa wa Primus League Burundi mwaka huu wa michezo 2024-25".
Nchini Burundi inabaki wiki moja ya mchezo kabla ya kutamatika kwa ligi msimu huu wa 2024-25.
Christopher Karenzi, DW Kigali