APR kwenye droo na mabingwa wa Afrika Pyramids
11 Agosti 2025Timu hizi zitakazowakilisha Rwanda kwenye mashindano yote ya Afrika zitanzia hatua ya awali, ambapo APR FC itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ya CAF na kukutana na Pyramids ya Misri katika michezo itakayofanyika kati ya Septemba 19–21, 2025, huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa wiki moja baadaye.
Licha ya kuwa Pyramids ndiyo mshindi mtetezi, hii ni mara ya tatu mfululizo timu hizi kukutana, lakini safari hii ni katika hatua ya kwanza ya awali.
Baadhi ya mashabiki wa APR wanahofia kukutana kwa mara nyingine tena na timu hiyo.
APR FC wametolewa mara mbili mfululizo na Pyramids FCkatika hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika msimu uliopita, timu hiyo kutoka Misri iliiondoa mabingwa wa Rwanda katika raundi ya pili kwa jumla ya magoli 4-2 za APR na hatimaye ikaibuka mabingwa wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Mwenyekiti wa Heshima wa APR FC, Jenerali Mubarakh Muganga, akiongea na vyombo vya habari amesema timu ya APR inaweza kuwaondoa Pyramids FC katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, Jenerali Muganga amesema kuwa hana shaka kuwa safari hii Wamisri hao wataondolewa.
Muganga anakiri kuwa haikuwa droo nzuri kwa APR, lakini pia ameonya kuwa matokeo yanaweza kuwa tofauti safari hii.
"Hii si droo mbaya pia, na nataka niwaambie kuwa timu yetu inaweza kuwaondoa Pyramids FC. Hivyo basi, mashabiki wa APR FC, msivunjike moyo," alisema.
Mafanikio yahitaji kujipanga
Kocha mkuu wa Aigle Noirs FC Jimmy Ndayizeye akichambua kuhusu mchuano huo kati ya mabingwa hao, amesema Pyramids ni timu kali mabingwa watetezi wa Afrika lakini APR wanaweza kujipanga vizuri wakaiondoa. Eti kwenye mchezo wa soka kila kitu kinawezekana.
Kocha Ndayizeye amesema " Waarabu wanapokuwa ugenini wanacheza kwa kujihami na kutafuta sare yoyote ile. Wanapofika kwenye uwanja wao wanafanya ushambulizi wa hapa na pale na kukuletea presha.
Wakipata mabao mawili au matatu, tayari wanakuwa wamejiandalia mazingira mazuri ya kukuondoa''.
Hayo yakijiri nchini Rwanda, timu ya Rayon sports itaipokea Yanga SC katika kilele cha siku kuu maarufu ‘' Rayon day'' mechi ambayo itapigwa katika uwanja wa Taifa wa Amahoro, jijini Kigali. Rayon ni mwakilishi wa Kombe la shirikisho la ligi barani Afrika CAF Confederation Cup.
Mashabiki wengi wa Yanga kutoka nchini Tanzania wanaanza safari yao kuanza jumatano wiki hii kuja Kigali kujionea mtanange huo wa mwende mkaone.
Kwa upande mwingine Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Rwanda APR imeandaa shindano la mechi za kujipima nguvu, litazozileta kwa pamoja mabingwa wa ligi ya Zambia Power Dynamos, Polisi ya Rwanda na AS Kigali.
Christopher Karenzi, DW Kigali