ANKARA:Rais Assad azuru Uturuki
7 Januari 2004Matangazo
Rais Bashar el Assad wa Syria amekutana na Rais Necdet Sezer wa Uturuki mjini Ankara. Assad ni kiongozi wa nchi wa kwanza wa Syria kuutembelea mji mkuu wa Uturuki tokea Syria ilipojipatia uhuru hapo mwaka 1946.Katika mkutano na waandishi wa habari Assad amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa utulivu Mashariki ya Kati na kutowa wito wa kupigwa marufuku kwa kwa silaha za nuklea katika eneo hilo zima ikiwa pamoja na Israel.Rais huyo wa Syria amesema amekubaliana na msimamo wa Uturuki wa kupinga kuwepo kwa taifa huru la Kurdistan kaskazini mwa Iraq. Uhusiano kati ya serikali ya Ankara na Damaskus umekuwa wa mvutano kwa miaka mingi kutokana na mzozo wa mpaka na madai kwamba Syria inawaunga mkono wanamgambo wa Kikurdish nchini Uturuki. Assad pia anatazamiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa mazungumzo juu ya uhusiano wa kiuchumi, ushirikiano wa usalama na mzozo kati ya Israel na Palestina.