ANKARA Watalii wa Uingereza wajeruhiwa katika shambulio la bomu nchini Uturuki
16 Julai 2005Wizara ya mambo ya kigeni nchini Uingereza imetangaza kwamba watalii watano wa Uingereza ni miongoni mwa majeruhi wa shambulio la bomu lililofanywa leo nchini Uturuki. Watu kadhaa waliuwawa katika shambulio hilo wakati mwanamke wa kujitoa muhanga mwenye umri wa miaka 20, alipojilipua akiwa ndani ya basi hilo katika mji wa mapumziko wa Kusadasi ulio karibu na baharini.
Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, amelitaja shambulio hilo kuwa la kigaidi. Gavana wa Kusadasi, Ali Baris, amesema mlipuko huo umewajeruhi watu 14, baadhi yao wakiwa mahututi. Juma lililopita watu kadhaa walijeruhiwa nchini humo katika shambulio lengine la bomu karibu na mji wa mapumziko wa Cesme, lililofanywa na kundi la waasi wa kikurdi, Kurdistan Liberation Hawks.