Andijan, Uzbekistan. Rais wa Uzbekistan akataa miito wa kufanyika uchunguzi huru kufuatia kuuwawa kwa raia kadha katika maandamano nchini mwake.
21 Mei 2005Rais wa Uzbekistan , Islam Karimov , amekataa miito ya kufanyika uchunguzi katika tukio la wiki iliyopita la kuzima maandamano katika eneo la mashariki ya nchi hiyo.
Jumuiya ya kimataifa imeitaka Uzbekistan kuruhusu uchunguzi huru wa kimataifa kuhusiana na ripoti kuwa majeshi ya usalama ya nchi hiyo yamefyatua risasi na kuwauwa mamia ya waandamanaji waliokuwa wakiipinga serikali.
Shirikisho la haki za binadamu lenye makao yake mjini Helsinki limesema kuwa kiasi cha raia 1,000 huenda wameuwawa katika miji ya Andijan na Pakhta-abad. Serikali ya Uzbekistan inakanusha taarifa hizo kuwa iliamuru majeshi yake kuwafyatulia risasi waandamanaji.
Serikali hiyo inasema kuwa watu 169 wamekufa katika kile inachosema kuwa ni mapambano kati ya Waislamu waliokuwa wakitaka kuipindua serikali na maafisa wa jeshi ambao walikuwa wakijaribu kurejesha hali ya utulivu.