Amri ya kutotoka nje yatangazwa kwenye kambi ya Kakuma
5 Machi 2025Marufuku hiyo itatekelezwa kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa moja asubuhi hadi pale hali itakapokuwa shwari. Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maandamano ya wakimbizi wanaolalimikia upungufu wa chakula na maji kambini humo.
Marufuku hiyo ilianza kutekelezwa jana jumanne katika kambi hiyo ya wakimbizi inayowasitiri zaidi ya wakimbizi laki mbili. Hali kambini humo imekuwa ya wasiwasi tangu siku ya Ijumaa wiki iliyopita, wakimbizi walipoingia barabarani kulalamikia mapungufu kadhaa ikiwemo uhaba wa chakula na maji miongoni mwa masuala mengine.
Karibu wakimbizi wanne wamejeruhiwa kwa risasi kufuatia makabiliano kati yao na polisi walipojaribu kuingia katika ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa wa kuwashugulikia Wakimbizi, UNHCR mjini Kakuma.
Wakimbizi wanadai maisha yamekuwa magumu kambini humo na sasa wanataka UNHCR iwape mwelekeo.
Aidha, wakimbizi hao wanaupinga mpango wa serikali ya Kenya kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa wa kuwashugulikia wakimbizi UNHCR wa kuwajumuisha na Wakenya kambini humo.
Wakimbizi wakabiliwa na hali ngumu, kiasi cha kusaka vibarua ili kujikimu
Wengi wanapinga mpango huo kwa kile wanachosema, watalazimika kutafuta vibarua kujikimu wakati Wakenya wenyewe wanahangika kupata ajira. Kulingana na wakimbizi hao, zoezi hilo lingekuwa la hiari bali si kushurutishwa.
"Kuna kuhamishwa kwa aina tofauti; kwa nguvu na ile mtu anaamua kuondoka. Lakini hapa tunatishiwa turudi nyumbani. Licha ya nchi yetu kuwa na msukosuko wa kiusalama, tuko tayari kurejea nyumbani kwa sababu hatutakubali kunyanyaswa," alisema mmoja ya wakimbizi.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP ambalo huwapa wakimbizi chakula, hufadhiliwa pakubwa na serikali ya Marekani, ingawa hali imekuwa ngumu tangu Rais Donald Trump alipotangaza kukatisha misaada ya kimataifa.
Mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita, WFP, ambalo linasimamia usambazaji wa chakula katika kambi hiyo ya wakimbizi ya Kakuma, lilisema kuwa mgao wa chakula katika kambi za wakimbizi ulikuwa katika kiwango cha chini cha asilimia 45 kutokana na vikwazo hivyo vya rasilimali.
Soma pia: Wakaazi Turkana wataka kambi za Kakuma na Daadab zisifungwe
Serikali ya Marekani imepunguza asilimia tisini ya misaada ya kimataifa hali ambayo imeziathiri sekta kadhaa ulimwenguni.
Endapo maandamano ya wakimbizi yataongezeka kunahofiwa kuwepo ukosefu wa usalama kwenye kambi hiyo ya wakimbizi.
Hadi sasa, UNHCR haijatoa tamko lolote kuhusu matukio hayo ila usalama umeimarishwa kwenye kambi hiyo ya wakimbizi.
Kenya ina kambi mbili za wakimbizi, Kakuma iliyoko jimboni Turkana na Daadab iliyoko jimboni Garissa.
Maelfu ya wakimbizi katika kambi hiyo, ambayo inawahifadhi watu waliokimbia migogoro na ukame kutoka nchi jirani za Sudan Kusini, Ethiopia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, waliandamana jana Jumatatu kupinga kuhusu mgao wa chakula kutokana na vikwazo vya ufadhili.