Amnesty: Msumbiji ilifanya ukandamizaji baada ya uchaguzi
17 Aprili 2025Katika taarifa yake iliyotolewa jana jioni. Amnesty International imewanukuu watetezi wa haki za binadamu nchini Msumbiji wanaodai kuwa wimbi hilo la maandamano na ukandamizaji wa polisi lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 300.
Shirika hilo limezitaka mamlaka za Msumbiji kuchunguza mauaji hayo na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulioshuhudiwa baada ya uchaguzi na limetoa mwito kwa wote walihusika kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Maelfu ya watu nchini Msumbiji walimiminika mitaani kwa majuma kadhaa baada ya uchaguzi wa rais na bunge wa Oktoba 9 mwaka jana ambao mwanasiasa wa chama tawala cha FRELIMO, Daniel Chapo alitangazwa mshindi wa kiti cha urais.
Maandamano hayo yalikuwa ni ya kumuunga mkono mgombea urais wa upande wa upinzani Venancio Mondlane aliyelalamika kwamba uchaguzi huo uligubikwa na dosari na madai ya wizi wa kura.