Amnesty International yataka udhibiti 'vifaa vya shoti'
6 Machi 2025Shirika hilo la uangalizi wa haki za binaadamu ulimwenguni lilisema siku ya Alkhamis (Machi 6) kuwa vifaa hivyo, ambavyo "kwa asili yake ni vya udhalilishaji", vinatumiwa na vyombo vya usalama kwa ajili ya mateso na ukatili kwenye mataifa ya China, Venezuela na Iran.
Ripoti ya shirika hilo lenye makao yake makuu London, Uingereza, iliyopewa jina la "Bado Siwezi Kulala Usiku - Matumizi Mabaya ya Vifaa vya Shoti ya Umeme" ilisema vifaa hivyo vya umeme ni sehemu ya maisha ya kawaida kwenye magereza, hospitali za wagonjwa wa akili, na vituo vya kuwapokea wakimbizi na wahamiaji mipakani mwa mataifa mengine kadhaa ulimwenguni.
Soma zaidi: Amnesty yataka udhibiti vifaa vinavyotumia shoti ya umeme
Paktrick Wilcken, mtafiti wa Amnesty International kwenye masuala ya kijeshi, usalama na polisi alisema shoti za umeme kutoka vifaa hivyo "husababisha ulemavu wa muda mrefu na matatizo ya kisaikolojia kwa wanaotendewa na wakati mwengine hata kifo."
Utafiti huo uliofanyika kwa kipindi cha miaka 10, kutoka mwaka 2014 hadi 2024 kwenye mataifa zaidi ya 40, uliangazia pia ongezeko la utumiaji wa vifaa hivyo kwenye ndege zisizo na rubani au makombora yanayoongozwa kwa mashine kutokea mbali, ambapo walengwa wake hupigwa kwa shoti za umeme zinazowafanya wasiweze kutembea.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo, vifaa hivyo vinaweza kutumika kisheria kwenye masuala ya usalama, lakini mara nyingi huwa vinatumika kinyume na sheria, vikiwemo visa vya kutumika bila ulazima na au kutumika kibaguzi.
Marufuku ya utengezaji, usambazaji na matumizi
Amnesty International ilitaka pawepo marufuku ya kukutanisha kifaa cha umeme moja kwa moja kwenye mwili wa mtuhumiwa na vifaa vinavyotumika kwenye ndege zisizo rubani viruhusiwe tu pale panapohakikishwa kuna udhibiti wa kutosha ili visitumike kuvunja haki za binaadamu.
Kwa sasa, licha ya kuwepo hatari za wazi za vifaa hivyo, hakuna kanuni za kilimwengu zinazodhibiti utengezaji na biashara yake, limesema shirika hilo.
Soma zaidi: Amnesty International yaishtumu Israel kwa mauaji ya halaiki katika ukanda wa Gaza
Ushahidi uliokusanywa kutoka kwa waathirika wa mateso waliyofanyiwa kwa vifaa hivyo maeneo mbalimbali ulimwenguni unaonesha wengi walipata majeraha makubwa kwenye mafuvu, macho, viungo vya ndani na sehemu za siri, na pia ngozi iliyounguwa, mipasuko, au mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida.
Utafiti huo uligunduwa kuna kampuni 197, nyingi yao zikiwa China, India na Marekani, ambazo zinajihusisha na utengenezaji na usambazaji wa vifaa hivyo kwa vyombo vya usalama.
Kampuni ya Kimarekani, Axon, ilisema vifaa vyake chapa TASER, ambavyo ndivyo vilivyosambaa kwa wingi zaidi, vinatumiwa na zaidi ya mashirika 180,000 ya usalama kwenye zaidi ya nchi 80 duniani.
Kwa kushirikiana na mashirika mengine zaidi ya 80 ulimwenguni, Amnesty International ilitaka kuwepo kwa kile inachokiita "mkataba wa kimataifa wa biashara isiyo na mateso" ili kudhibiti biashara na matumizi ya vifaa hivyo miongoni mwa vyombo vya usalama.
AFP