Amnesty yakosoa bomoa bomoa ya makaazi Ethiopia
14 Aprili 2025Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, limesema leo kwamba Ethiopia inaendesha mchakato wa kuhamisha kwa nguvu idadi kubwa ya watu na imeshindwa kuzishauri familia zilizoathirika na zoezi hilo.
Shirika hilo limeitolea mwito serikali ya mjini Addis Ababa kusitisha mara moja mchakato huo wa miradi ya kuifanyia ukarabati miji.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliyeingia madarakani 2018 anaongoza kile kinachofahamika kama mradi wa barabara, unaolenga kuzikarabati na kutanua barabara za mji mkuu na miji mingine ya taifa hilo.Soma pia: Abiy akabiliwa na changamoto kubwa Ethiopia
Tangu alipoanzisha mradi huo mwaka 2022 kumeshuhudiwa hatua za kubomolewa majumba, maduka na majengo ya maofisi katika mji mkuu, Adis Ababa, na miji mingine kiasi 58.
Amnesty International imeiomba serikali kusitisha hatua ya kuhamisha watu na mradi huo hadi itakapofanyika tathmini ya kuangalia athari zake kwa haki za binadamu.