Amnesty International yailaumu M23
27 Mei 2025Amnesty International imewatuhumu waasi hao wa M23 katika eneo la mashariki mwa Kongo kwa kuua, kuwatesa, kuwateka na kuwatokomeza kusikojulikana raia waliokuwa mahabusu kutoka kwenye miji miwili inayodhibitiwa na waasi hao.
Amnesty International katika taarifa yake imesema "vitendo hivi vinakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu na vinaweza kuchukuliwa kuwa sawa na uhalifu wa kivita.”
Soma pia: Pande zote kwenye vita vya Kongo huenda zimekiuka sheria ya vita
Mzozo wa Kongo, uliongezeka mnamo mwezi Januari, wakati kundi la M23 lilipopata nguvu zaidi na kusonga mbele hadi kuuteka mji wa kimkakati wa Goma katika jimbo la Kivu Kaskazini, na kisha mji wa Bukavu mwezi uliofuata wa Februari.
Kulingana na shirika hilo, kati ya Februari na mwezi Aprili, liliwahoji raia 18 waliokuwa wamezuiliwa na M23 huko Goma na Bukavu, baada ya kutuhumiwa kuliunga mkono jeshi au serikali ya Kongo. Wafungwa hao wa zamani wamesema waasi hawakutoa ushahidi wowote wa tuhuma hizo na wala hawakufahamishwa sababu za wao kuwekwa kizuizini.
Baadhi ya watu waliozuiliuwa wameelezea jinsi walivyowashuhudia waasi wa M23 wakiwaua wafungwa wenzao wawili kwa kumpiga nyundo mmoja na kwa kumpiga risasi mwingine aliyekufa papo hapo.
Soma pia: DR Kongo, M23 watoa ahadi ya pamoja kufikia mapatano
Wafungwa wote wa zamani waliohojiwa na shirika la Amnesty International wamesema waliteswa na waliwashuhudia wapiganaji wa M23 wakiwatesa wafungwa wengine ndani ya magereza walikozuiwa wamesema baadhi yao walipigwa viboko kwa kutumia vipande vya mbao, nyaya za umeme au hata mikanda. Wamesema waliwaona wafungwa wenzao wakifariki kutokana na hali ngumu, na mateso.
Taarifa ya Amnesty International imeelezea kuwa wafungwa hao wa zamani walizuiliwa katika seli zilizojaa, chafu, na bila kupewa chakula cha kutosha, maji, vifaa vya kutumia vyooni au huduma za afya.
Kwa mujibu wa Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, jamaa walihangaika kuwatafuta wapendwa wao kote magezrezani na katika vizuizi vingine, na wapiganaji wa M23 mara nyingi walikataa kuwapa taarifa iwapo jamaa zao walikuwa huko, hali ambayo Amnesty International imesema ni sawa na kuzilazimisha jamaa za watu hao kukubali kwamba wapendwa wao wametoweka.
M23 ni mojawapo ya makundi yapatayo 100 yanayo miliki silaha na ambayo yamekuwa yakipigania udhibiti wa eneo lenye utajiri wa madini huko Mashariki mwa Kongo ambalo liko katika mpaka kati ya Kongo na Rwanda, mzozo huo ni mmojawapo kati ya mizozo mikubwa inayoendelea ulimwenguni na ambao umesababisha mgogoro ya kibinadamu.
Zaidi ya watu milioni 7 wamlazimika kuyakimbia makazi yao, wakiwemo watu 100,000 walioyakimbia makazi yao mnamo mwaka huu (2025).
Soma pia: Tetesi za Kabila kuwasili Goma zazusha mivutano Kongo
Kulingana na watalaamu wa Umoja wa Mataifa, waasi hao wanaungwa mkono na takriban wanajeshi 4,000 kutoka nchi jirani ya Rwanda na wakati fulani walitishia kwamba wangeingia hadi kwenye mji mkuu wa Kongo, Kinshasa, ulio karibu kilomita 1,600 kutoka upande wa mashariki ya nchi hiyo.
Licha ya jeshi la Kongo na M23 kufikia makubaliano na kukubali kuyafanyia kazi mapatano hayo yaliyofikiwa mwezi uliopita, mapigano kati ya pande hizo mbili bado yanaendelea.
Chanzo:AP