Amnesty International: GHF yatumika kuwauwa Wapalestina
4 Julai 2025Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, jumla ya Wapalestina 300 wameuawa ndani ya kipindi cha masaa 48 yaliyopita kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel kwenye Ukanda wa Gaza, wengi wao wakiwa kwenye kusaka chakula karibu na vituo vya usambazaji misaada vya Wakfu wa Kibinaadamu wa Gaza (GHF), ambao wakosoaji wanauita 'usio wa kibinaadamu'.
Jeshi la Israel linadai kuwa kuanzia Jumatano (Julai 2), limeyashambulia maeneo 150 kwenye Ukanda huo, yakiwemo makundi linayoyaita ya kigaidi na mahandaki wanayotumia.
Miongoni mwa waliouawa kwenye mashambulizi hayo ya anga, linavyodai jeshi hilo, ni wale waliohusika na urushaji kombora kuelekea Israel siku ya Jumatano.
Hata hivyo, shirika la habari la Ujerumani, dpa, halikuweza kuthibitisha madai hayo kupitia vyanzo huru.
GHF ni mtego wa mauti?
Lakini shirika la haki za binaadamu la Amnesty International limeutuhumu mfumo mzima wa usambazaji misaada unaoungwa mkono na Marekani na Israel kwa "kutumia njaa kama mbinu ya kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza."
Wizara ya Afya ya Gaza imesema zaidi ya Wapalestina 500 wameuawa kwenye ama karibu na vituo vya usambazaji vya GHF ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Vituo hivyo vinalindwa na walinzi wa kampuni za kibinafsi na vimejengwa karibu na maeneo ya kijeshi ya Israel, ambapo mara kwa mara walinzi hao na wanajeshi wa Israel wamekuwa wakiwarushia risasi ovyo ovyo raia wanaosaka msaada wa chakula.
Kwenye ripoti yake iliyosambazwa siku ya Alkhamis (Julai 3), Amnesty International ilisema Israel imegeuza hali ya kusaka misaada kuwa "mtego wa kuwanasa Wapalestina wanaokufa njaa kupitia vituo vinavyodhibitiwa kijeshi vya GHF."
Shirika hilo la haki za binaadamu lilisisitiza kwamba hali iliyotengenezwa imeunda mchanganyiko hatari wa njaa na maradhi unaowasukuma watu kwenye maangamizo.
Katibu mkuu wa Amnesty International, Agnes Callamard, alisema "kupotezwa kwa maisha ya watu kunaonekana kama lengo la makusudi la jeshi la Israel na matokeo yaliyofahamika mapema kwa kuwa na mfumo wa aina hii wa usambazaji misaada."
Walinzi wa GHF wakiri kuuwa
Katika mahojiano maalum na shirika la habari la Associated Press, baadhi ya walinzi binafsi wanaofanya kazi na shirika la GHF walikiri kwamba wamekuwa wakiwarushia risasi ovyo ovyo watu wanaokwenda kwenye vituo hivyo kusaka msaada wa chakula.
Hata hivyo, shirika la GHF limekanusha taarifa hiyo likidai halina walinzi wenye silaha, na kwamba milio ya risasi inayotajwa kwenye ripoti hiyo ni ya jeshi la Israel.
Ripoti ya Amensty International inafuatia tamko lililotolewa wiki hii na zaidi ya mashirika 160 makubwa ya kimataifa ambayo ilitowa wito wa kusitishwa mara moja kwa shirika la GHF.
Kama ilivyokuwa kwa Amnesty International, mashirika hayo nayo yalihoji kwamba mfumo mzima wa GHF unairuhusu Israel kutumia chakula kama silaha, unavunja misingi ya misaada ya kiutu na hauna ufanisi wowote.
Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje wa Israel imeikanusha ripoti hiyo ya Amnesty International ikirejelea shutuma zake kwa wakosoaji kwamba wanaungana na kundi la Hamas kuendeleza propaganda na kundi hilo