Albanese asema Netanyahu anafumbia macho hali halisi ya Gaza
12 Agosti 2025Albanese ameyasema hayo siku moja baada ya kutangaza kwamba Australia itaitambua Palestina kama dola ifikapo mwezi septemba
Albanese amesema hatua ya serikali ya Netanyahu kusita kuwasikiliza washirika wake ndio iliyosababisha Australia kufikia uamuzi wa kuitambua Palestina kama dola.
"Vurugu zimeendelea tangu 2023, tangu Oktoba 7, na mkakati wa serikali ya Netanyahu ni kuendelea, kufanya hali kuwa mbaya zaidi na kuiteka Gaza. Tayari inayakalia maeneo makubwa ya Gaza, Inaunga mkono ongezeko la makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi. Tunachohitaji kufanya ni kufanya kitu tofauti. Jumuiya ya kimataifa inasema inataka amani na usalama kwa wote Waisraeli na Wapalestina.''
Australia yatangaza kulitambua dola la Palestina
Australia ilitangaza jana kwamba itaitambua Palestina kwenye mkutano wa Hadhara Kuu wa Umoja wa Mataifa, hatua inayozidhisha shinikizo la kimataifa kwa Israel kusitisha vita Gaza baada ya Ufaransa, Uingereza na Canada kutangaza msimamo sawa na huo.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Johann Wadephul, ameunga mkono uamuzi wa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz kusitisha kwa sehemu mauzo ya silaha kwa Israel akisema hatua hiyo ni ya haki na inayokubalika.