Albanese amshutumu Netanyahu kwa hali ya Gaza
12 Agosti 2025Albanese ameyasema haya katikati mwa ongezeko la shinikizo la kimataifa la kuitaka Israel kumaliza vita vyake dhidi ya Hamas, na janga la kibinadamu lililougutua ulimwengu na kuyasukuma mataifa kadhaa makubwa kutangaza nia ya kuitambua Palestina kama taifa huru.
Waziri Mkuu Albanese, amesema Netanyahu "anakataa ukweli” kuhusu hali ya kibinadamu Gaza, siku moja baada ya kutangaza kuwa Australia italitambua taifa la Palestina kwa mara ya kwanza.
Utambuzi wa Palestina kama dola Septemba
Hatua hiyo, inayotarajiwa kutangazwa rasmi mwezi ujao kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, inaongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel baada ya hatua kama hiyo kuchukuliwa na Ufaransa, Uingereza na Canada.
"Vurugu zimeendelea tangu mwaka 2023, tangu tarehe 7 Oktoba, na mkakati wa serikali ya Netanyahu ni kuendelea tu, kuendelea kufanya yale yale, kulikalia jiji la Gaza. Tayari inaikalia sehemu kubwa za Gaza. Inasaidia ongezeko la makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi. Inajihusisha na vurugu za walowezi zinazoungwa mkono na mamlaka za Israeli katika Ukingo wa Magharibi. Tunaona mambo yale yale yakirudiwa.Tunachohitaji kufanya ni kufanya jambo tofauti. Jumuiya ya kimataifa inasema kwamba tunataka amani na usalama kwa Waisraeli na Wapalestina wote,” alisema Albanese.
Huku hayo yakijiri, Wizara ya Afya ya Gaza imesema watu wasiopungua 55 wameuawa katika mashambulizi ya Israel kuanzia usiku wa kuamkia Jumatatu, wakiwemo zaidi ya 15 waliokuwa wakisubiri msaada katika kivuko cha Zikim na wengine 12 waliouawa wakijaribu kufika kwenye maeneo ya ugawaji misaada.
Mashirika ya misaada yanasema mauaji ya watu wanaotafuta msaada yamegeuka kuwa matukio ya kila siku.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, ameunga mkono uamuzi wa Kansela Friedrich Merz wa kusitisha kwa sehemu mauzo ya silaha kwa Israel, akisema inalenga kutoa ishara ya kisiasa baada ya Israel kuidhinisha hatua ya kuukamata mji wa Gaza.
Wimbi la ukosoaji wa Israel limeongezeka baada ya shambulizi lililoua timu ya waandishi wa Al Jazeera mjini Gaza, akiwemo mwandishi maarufu Anas al-Sharif na wenzake wanne.
Mauaji yakiuka sheria za kimataifa
Israel inadai Sharif alikuwa mwanamgambo wa Hamas, lakini Al Jazeera imepinga vikali madai hayo, ikisema lilikuwa jaribio la kukandamiza sauti za waandishi.
Mashirika ya kimataifa ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari yamesema mauaji hayo yanakiuka sheria za kimataifa, huku Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka, RSF, likiripoti karibu waandishi 200 wameuawa tangu Oktoba 2023.
Katika hatua nyingine, nyota wa muziki wa pop Madonna amemuhimiza kiongozi wa kanisa Katoli duniani, Papa Leo wa XIV kuutembelea Ukanda wa Gaza, akisema yeye pekee ndiye hatazuiwa kuingia na kutoa wito kwa milango ya misaada kufunguliwa ili kuwaokoa watoto wanaokumbwa na njaa.
Akiadhimisha siku ya kuzaliwa ya miaka 25 ya mwanawe, Madona ameahidi kuchangia mashirika ya misaada, wakati ambapo takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa utapiamlo mkali kwa watoto Gaza umefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.